Hatimaye uongozi wa Tottenham Hotspurs umesitisha mkataba wa mshambuliaji kutoka nchini Togo Emmanuel Adebayor, baada ya kumuondoa kwenye orodha ya wachezaji waliosajiliwa kwa ajili ya michezo ya ligi ya mabingwa barani Ulaya pamoja na Europa League.

Uthibitisho wa kufanywa kwa maamuzi hayo ulitolewa jana jioni baada ya pande zote mbili kuwa na mazungumzo ya kina kwa siku kadhaa, na imebainika ni bora wakaachana kwa salama na kumpa nafasi Adebayor kusaka mahala pengine pa kupata mkate wake wa kila siku.

Adebayor, alikua na wakati mgumu wa kucheza soka tangu msimu uliopita, kufutia masuala la kifamilia yaliyokua yakimkabili, na alifikia hatua ya kuutaka uongozi wa klabu ya Spurs kumpa ruhusa ya kupumzika kwa muda.

Hata hivyo kabla ya dirisha la usajili wa majira ya kiangazi halijafungwa mwanzoni mwa mwezi huu, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31, alikua anakaribia kusajiliwa na klabu za Aston Villa pamoja na West Ham Utd lakini mambo yalikua magumu kwake kutokana na hitaji la mshahara mkubwa kwa juma.

Adebayor alipewa nafasi ya kuzungumza na viongozi wa klabu hizo mbili huku Spurs wakiamini huenda mambo yangekua mazuri, lakini walisikitishwa kutokana na maamuzi ya Adebayor ambaye alionyesha kuhitaji mshahara wa paund 100,000 kwa juma.

Kuvunjwa kwa mkataba wa Adebayor huko White Hart Lane kunampa uhuru wa kuwa na nafasi ya kujiunga na klabu yoyote kwa sasa, na kutokana na kanuni za ligi kuu ya soka nchini England, mshambuliaji huyo anaweza kusajiliwa katika kipindi hiki licha ya dirisha kufungwa mwanzoni mwa mwezi huu.

Kwa sasa Adebayor yupo nchini Ufaransa akitafakari kwa kina na amesisitiza kuwa tayari kufanya maamuzi ya kujiunga na klabu itakayoonyesha nia ya dhati ya kutaka kufanya nae kazi, wakati wowote mambo yatakapokua vizuri.

Inter Milan Kidume Cha Milan
JK Awapa CCM Mbinu Mpya Ya Kampeni Ya Ushindi