Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameshindwa tena kupata dhamana hivyo kulazimika kuukaribisha mwaka mpya akiwa gerezani, baada ya shauri lake la maombi ya dhamana kuahirishwa jana katika Mahakama Kuu kanda ya Arusha.

Mahakama hiyo ililazimika kuahirisha kusikiliza shauri la maombi ya dhamana ya Lema baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha mahakamani hapo notisi ya kupinga uamuzi wa mahakama hiyo wa kumuongezea muda wa kukata rufaa ili apate dhamana.

Kutokana na hatua hiyo, Lema alirejeshwa tena mahabusu hadi Januari 4 mwakani kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo kwa ajili ya kutolewa maamuzi.

Awali, Jaji Dk. Modesta Opiyo alitupilia mbali pingamizi la Jamhuri na kukubali maombi ya upande wa Lema ya kuongezewa muda wa kukata rufaa akieleza kuwa uamuzi huo ulitakiwa kuzingatia busara zaidi ili mtuhumiwa apate haki yake ya dhamana.

Lema anakamilisha miezi miwili ndani ya mahabusu akikabiliwa na kesi ya uchochezi na kutoa lugha ya maudhi dhidi ya Rais John Magufuli. Alikamatwa na kuwekwa rumande tangu Novemba 2 mwaka huu.

Jaji Salma Maghimbi ambaye jana alikuwa akisikiliza shauri hilo, aliamuru upande wa Jamhuri kuwasilisha hoja zake za kupinga upande wa utetezi kuongezewa muda wa kukata rufaa na kuutaka upande wa utetezi kuzijibu haraka ili majumuisho yafanywe Januari 3 mwakani na uamuzi kutolewa Januari 4.

Wadaiwa sugu elimu ya juu kusakwa nyumba nyumba
Zahor: Asante 'President', Ila….