Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ametolea ufafanuzi suala la matibabu ya mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Antiphas Lissu aliyepelekwa Nairobi nchini Kenya baada ya kupigwa risasi.

Ndugai amesema kuwa utaratibu wa matibabu kwa mbunge yeyote ulikuwa umeshafuatwa lakini familia iliomba yenyewe kumpeleka Nairobi, na siyo kama walishindwa kumpeleka nchini India

“Baada ya bunge kupata taarifa kuhusu tatizo hilo, sisi bunge tulikuwa tumeshaagiza ndege tayari ilikuwa uwanjani, hapa Dodoma kwa ajili ya kumpeleka Hospitali ya Muhimbili ambapo ndiyo utaratibu wa kibunge, na kama kuna rufaa ya nje ya nchi utaratibu wetu ni kwamba serikali yetu ina mkataba na hospitali ya Apolo kule India,”amesema Ndugai

Aidha, Ndugai ameongeza kuwa Lissu alipelekwa Nairobi Kenya kwa sababu familia iliomba ambapo walisema wangejisikia faraja kwao wenyewe kuchagua sehemu ya kumpeleka kutibiwa.

Hata hivyo, Ndugai amesema kuwa tukio la kupigwa risasi kwa Tundu Lissu ni la kwanza tangu historia ya bunge kuhamia Dodoma kwa miaka mingi, na kuvitaka vyombo vya dola kushughulikia tatizo hilo.

Ni bora tuifunge kuliko kuendelea kuibiwa- JPM
FIFA yawarudisha uwanjani Senegal na Afrika Kusini