Baada ya kuteuliwa na CCM na kupita katika mchakato wa kumpata mgombea Uspika wa Bunge la Kumi na moja bila kupingwa, Job Ndugai ameeleza changamoto anazotarajia kukutana nazo ikiwa ni pamoja na migomo.

Akiongea na waandishi wa habari jana baada ya jina lake kupitishwa, Ndugai alilielezea Bunge la kumi na moja kama Bunge lenye utofauti mkubwa na mabunge mengine huku akidai kuwa ongozeko la vijana wengi na wasomi wengi zaidi kunaashiria kuongezeka kwa changamoto zaidi.

“Bunge hili lina wabunge wengi vijana, lina wabunge wengi wasomi zaidi kuliko mabunge yote yaliyowahi kutokea na lina uwakilishi mkubwa. Hili ni Bunge ambalo litakuwa na changamoto nyingi, tetegemee migomo ya hapa na pale, hata hivyo ubora wa kazi utakuwa mkubwa,” alisema Ndugai.

Hata hivyo, Ndugai alisisisitiza kuwa ataliongoza Bunge kwa weledi na kutenda haki kwa kila upande hivyo aliwataka wabunge wote wakiwemo wa upinzani kumuunga mkono leo ili awe Spika wa Bunge la 11.

Ndugai anatarajia kuchuana na wabunge wengine wa upinzani ambapo mshindani wake mkuu anatarajiwa kuwa Goodluck Ole Mideye, ambaye anaungwa mkono na vyama vinne vya upinzani vinavyounda Ukawa.

Kwa upande mwingine, taarifa kutoka mjini Dodoma zinaeleza kuwa Mbunge wa kuteuliwa, Dkt. Tulia Ackson aliyekuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali anaandaliwa na CCM kuwa Naibu Spika wa Bunge hilo ambapo atapigiwa kura na wabunge akichuana na Magdalena Sakaya wa CUF anayeungwa mkono na Ukawa.

 

Majanga Yarejea Tena Muhimbili Baada ya Rais Kuyaondoa
Lambert Akabidhiwa Kikosi Cha Rovers