Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inatarajia kufanya zoezi la uandikishaji wa Wapiga Kura kwa majaribio katika Kata mbili za Kibuta iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani na Kihonda katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Mkoani Morogoro.
 
Katika taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume Jaji (Rufaa), Semistocles Kaijage Jijini Dar es Salaam imesema kuwa Uandikishaji huo wa Majaribio utakaoanza Machi 29, hadi Aprili 04, 2019 utafanyika katika vituo 20 vya kuandikisha Wapiga Kura ikiwa ni vituo 10 katika kila Kata.
 
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uandikishaji huo unalenga katika kuvifanyia majaribio vifaa na mfumo wa Uandikishaji Wapiga Kura ili kubaini changamoto kabla ya kuanza rasmi kwa zoezi hilo.
 
Aidha, imesema kuwa uandikishaji huo hautawahusu raia walio chini ya kiapo cha utii wa nchi nyingine, aliyebainika kuwa hana akili timamu au yuko kizuizini kama mhalifu mwenye ugonjwa wa akili au yuko kizuizini kwa ridhaa ya Rais.
 
Pia taarifa hiyo imeendelea kutaja watu ambao hawatahusika katika majaribio hayo ya uboreshaji kuwa ni mtu aliyehukumiwa adhabu ya kifo na mahakama au anatumikia kifungo kinachozidi miezi sita pamoja na mtu aliyepoteza sifa za kuandikishwa kuwa Mpiga Kura chini ya Sheria za Uchaguzi au Sheria nyingine yoyote inayohusu makosa ya uchaguzi.
 
Vile vile, Tume imevitaka Vyama vyenye nia ya kuweka Mawakala katika uandikishaji huu wa Majaribio kuwasilisha orodha ya majina ya Mawakala na vituo walivyopangiwa kwa Maafisa Waandikishaji wa Halmashauri za Kisarawe na Manispaa ya Morogoro.
 
Kadhalika Vyama vimetakiwa kuwasilisha nakala mbili za barua za utambulisho zikiwa na picha mbili na nakala mojawapo kati ya Kitambulisho cha Taifa au Kadi ya Mpiga Kura, Pasi ya Kusafiria au Leseni ya Udereva na kwamba kila Chama kitagharamia Wakala wake.
 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi hufanya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mujibu wa Ibara ya 74 (6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoipa Tume mamlaka ya kusimamia na kuratibu uandikishaji wa Wapiga Kura katika Uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano pamoja na Madiwani kwa Tanzania Bara.
 
  • JPM atengua, ateua mwingine TAA
 
  • LIVE: Waziri Mwakyembe akizungumza kwenye Jukwaa laFursa za Biashara na Uwekezaji Mkoani Lindi
 
  • ACT- Wazalendo wapewa siku 14, ‘Jielezeni kwanini chama chenu tusikifute?
 
Kwa mujibu wa Kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Kifungu cha 21(5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292 Tume inapaswa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya Uchaguzi Mkuu mmoja na unaofuata

Wa kwanza Timu Maalim Seif apewa uongozi ACT-Wazalendo
JPM atengua, ateua mwingine TAA