Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekishauri Chama cha Wananchi (CUF) kumaliza mgogoro unaoendelea ndani ya Chama hicho kwani unaweza kusababisha kupoteza nafasi za Udiwani katika Uchaguzi Mdogo unaotarajiwa kufanyika wakati wowote kuanzia sasa.

Hayo yamesemwa mapema hii leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo. Kailima Ramadhani alipokuwa akijibu tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa kwa Tume hiyo ikiwemo suala la Uteuzi wa Wabunge wa Viti Maalum kupitia CUF.

Amesema kuwa mvutano unaoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) haunatija, hivyo ameshauri pande mbili zinazovutana kukutana na kumaliza tofauti zao kwani hali hiyo inaweza kuwanyima nafasi ya kutoa wagombea kwenye uchaguzi huo mdogo.

‘‘Mimi niwashauri,CUF wanamgogoro wao wamalize mgogoro wao. Ni vizuri wakutane wamalize mgogoro wao kwani hii inaweza kuwaletea matatizo wagombea wakati wa Uchaguzi.’’ amesema Kailima.

Aidha amesema kuwa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, inakitaka Chama cha Siasa kumsimamisha Mgombea mmoja kwa nafasi moja, lakini pia mgombea wa nafasi ya Rais na Mbunge lazima fomu yake isainiwe na Viongozi wa ngazi ya Taifa wanaotambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.

Hata hivyo, Kailima ameongeza kuwa  Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatambua taarifa za Vyama vya Siasa iliyowasilishwa naMsajili wa Vyama vya Siasa na kwa Chama cha CUF viongozi wanaotambuliwa na Tume hadi hivi sasa ni Mwenyekiti Prof. Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad.

 

Tanesco waigomea bomoabomoa Kimara
Manula kuchezea rasmi klabu ya Simba