Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), Jaji Damian Lubuva leo ametoa msimamo rasmi wa Tume hiyo kuhusu uchaguzi wa Jimbo la Kijitoupele visiwani Zanzibar, jimbo ambalo halikufanya uchaguzi Oktoba 25 mwaka jana.

Akiongea na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Hotel ya Zanzibar Beach Resort, Jaji Lubuva amesema kuwa Tume ya Uchaguzi itasimamia uchaguzi wa jimbo hilo kama ilivyokuwa kwa majimbo mengine mwaka jana kwakuwa uchaguzi wake ulisimamishwa kabla ya tangazo la kufutwa kwa uchaguzi lililotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Kijitoupele ni jimbo moja kati ya majimbo 264 ya uchaguzi, hivyo kukamilika kwa uchaguzi huo kesho kutakamilisha idadi kamili ya majimbo yote yaliyo chini ya NEC.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa NEC, Kailima Ramadhani alikiri kupokea barua ya Chama Cha Wananchi (CUF) kujitoa katika uchaguzi huo lakini aliungana na kauli iliyowahi kutolewa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kuwa chama hicho hakikufuata kanuni na taratibu za kujitoa.

“Ni kweli CUF wametuletea taarifa ya kujitoa katika Uchaguzi wa Jimbo la Kijitoupele lakini hawakufuata taratibu na kanuni hivyo basi taarifa yao ni batili na NEC haitambui kujitoa kwao,” alisema Kailima.

NEC imetoa wito kwa wananchi visiwani Zanzibar kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi huo wa marudio.

Ndege kubwa yaanguka na kuua makumi
Chidi Benz aweka wazi kinachomkondesha, aomba msaada