Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza Tarehe ya uchaguzi katika majimbo ya Simanjiro na Serengeti pamoja na kata 21 za Tanzania Bara ambapo unatarajiwa kufanyika Desemba 2, 2018 mwaka huu.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage ambapo amesema kuwa fomu za Uteuzi wa Wagombea zitatolewa kati ya tarehe 28 Oktoba hadi 03 Novemba mwaka huu.

“Uteuzi wa Wagombea utafanyika tarehe 03 Novemba mwaka huu. Kampeni za Uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 04 Novemba hadi tarehe 01 Desemba mwaka huu na siku ya Uchaguzi itakuwa ni tarehe 2 Desemba, mwaka huu,” amesema Jaji Kaijage.

Amesema kuwa Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, aliitaarifu tume uwepo wa nafasi za wazi za Ubunge katika Majimbo mawili (2), Jimbo la Serengeti lililopo Halmashauri ya Serengeti Mkoani Mara na Jimbo la Simanjiro lililopo Halmashauri ya Simanjiro Mkoani Manyara.

Aidha, Kaijage amesema kuwa barua hiyo imepokelewa kufuatia Wabunge wa Majimbo hayo ambao ni Marwa Ryoba Chacha,  na James Ole Millya kujiuzulu na kutoka  kwenye vyama vyao vya awali.

Amesema Tume pia imepokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa ambaye kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika Kata 21 za Tanzania Bara. ambapo nafasi hizo wazi zimetokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo na kujiuzulu.

Hata hivyo, amezitaja kata zenye uchaguzi na halmashauri zake kwenye mabano ambapo ni pamoja na Ilboru, Mlanfarini na Oldonyosambu (Wilaya ya Arusha), Engutoto na Olasiti (Manispaa ya Arusha), Hazina (Manispaa ya Dodoma), Chinugulu (Wilaya ya Chamwino), Kasharu, Nyakimbili, Kishongo (Wilaya ya Bukoba), Chonyonyo, Ihanda (Wilaya ya Karagwe).

Nyingine ni pamoja na Muhindawa, Mnanila (Wilaya ya Buhigwe), Mnerongongo (Wilaya ya Nachingwea) Ngarenairobi (Wilaya ya Siha), Kyanyari (Wilaya ya Butiama), Namilembe (Wilaya ya Ukerewe), Lukanga, Beta (Wilaya ya Mkuranga) na Chikola (Wilaya ya Manyoni)

Midundo ya Afrika yampagawisha Kanye West
Video: Kazi bado nzito, Wabunge wawili Chadema, Meya hapatoshi, Mgombea CUF alia rafu Liwale