Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo kwenye jimbo la Babati Mjini mkoani Manyara na jimbo la Ukerewe lilipo jijini Mwanza pamoja na kata 26 za Tanzania Bara.

Taarifa iliyotolewa kwa umma na Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salum Mbarouk imesema kuwa uchaguzi huo utafanyika sambamba na uchaguzi wa Jimbo la Simanjiro na Serengeti pamoja na kata 21 za Tanzania Bara uliotangazwa awali.

“Nafasi hizo wazi zimetokana na waliokuwa Wabunge wa Majimbo hayo, Joseph Michael Mkundi (Ukerewe) na Pauline Philipo Gekul (Babati Mjini) kujiuzulu kutoka kwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),” amesema Jaji Mbarouk.

Amefafanua kuwa Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi ya Ubunge katika Majimbo hayo mawili.

Aidha, amesema kuwa fomu za uteuzi  wa  wagombea zitatolewa kati ya tarehe 28 Oktoba hadi 3 Novemba mwaka huu, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 3 Novemba mwaka huu, kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 4 Novemba  hadi tarehe 1 Desemba mwaka huu na siku ya uchaguzi itakuwa ni tarehe 2 Desemba, mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Jaji Mbarouk amesema Tume imepokea taarifa kutoka kwa waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa ambaye kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika Kata 26 za Tanzania Bara.

Ameongeza kuwa kwa  kuzingatia matakwa ya kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, pamoja na kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatoa taarifa kwa Umma kuhusu uwepo wa Uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Majimbo ya Babati Mjini na Ukerewe pamoja na Udiwani katika Kata Ishirini na Sita (26) za Tanzania Bara.

Majina ya Halmashauri na Kata zenye uchaguzi kwenye mabano ni kama ifuatavyo, Halmashauri ya Wilaya ya Temeke (Mtoni), Halmashauri ya Manispaa ya Ilala (Mnyamani), Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa (Salanka), Halmashauri ya Wilaya ya Magu (Kabila), Halmashauri ya Misungwi (Sumbugu, Buhingo), Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe (Bukiko), Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (Miteja, Kivinje, Singino, Somanga na Mitole).

Nyingine ni Halmashauri ya Wilaya ya Songea (Matarawe, Ruvuma), Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa (Mtipwili), Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti (Magange, Ring’wani, Rung’abure, Natta na Rigicha), Halmashauri ya Mji wa Babati (Maisaka), Halmashauri ya Wilaya ya Meru (Nkoanekoli), na Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti (Salale).

Video: Mo asakwa nyumba kwa nyumba Masaki, Kubenea, Komu sasa njiapanda, Mvua kubwa yaja
TMA yatoa tahadhari kwa wananchi kuhusu mvua kubwa