Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza ratiba ya Uchaguzi Mdogo katika majimbo ya Singida Kaskazini, Longido na Songea Mjini na kata sita za Tanzania Bara ambao utafanyika tarehe 13 Januari mwaka 2018.

Akitoa taarifa kwa umma jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Hamid Mahmoud Hamid, amesema Tume imetangaza uchaguzi huo kufuatia kupokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kuwepo nafasi wazi ya jimbo la Singida Kaskazini kufuatia kuvuliwa uanachama wa CCM mbunge wa jimbo hilo Lazaro Nyalandu na hivyo kupoteza sifa ya kuwa mbunge.

Kwa upande wa Jimbo la Songea Mjini, Jaji Hamid amesema kuwa Spika aliitaarifu Tume kuwepo nafasi wazi ya jimbo hilo kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Leonidas Gama huku Tume ikipokea Hati ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ikithibitisha kuwa Jimbo la Longido kuwa wazi baada ya kufuta matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo.

Ameongeza kuwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, aliitaarifu Tume kuwepo nafasi wazi za madiwani katika kata sita Tanzania Bara.

Jaji Hamid amezitaja kata zinazohusika katika uchaguzi huo kuwa ni Kimandolu (Halmashauri ya Jiji la Arusha), Kihesa (Halmashauri ya Manispaa ya Iringa), Bukumbi (Halmashauri ya Wilaya ya Uyui), Kurui (Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe), Keza (Halmashauri ya Wilaya ya Ngara) na Kwagunda (Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe).

Amesema utoaji fomu za uteuzi katika majimbo hayo na kata hizo sita utakuwa ni kati ya tarehe 12 hadi 18 Desemba, 2017 wakati katika jimbo la Songea Mjini utoaji fomu utakuwa kati ya tarehe 14 hadi 20 Desemba, 2017

Amefafanua kuwa kwa upande wa kampeni za uchaguzi huo katika majimbo ya Singida Kaskazini na Longido na kata zote sita zitaanza tarehe 19 Desemba, 2017 na kumalizika tarehe 12 Januari, 2018.

Katika jimbo la Songea Mjini, alisema kuwa kampeni za zitaanza tarehe 21 Desemba, 2017 na kumalizika tarehe 12 Januari, 2018 wakati siku ya uchaguzi katika majimbo yote matatu na kata zote sita itakuwa tarehe 13 Januari, 2018.

Jaji Hamid amevikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi wazingatie Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na Maelekezo yote wakati wa kipindi cha uchaguzi mdogo wa majimbo hayo na kata Sita.

Rais Karia Ashinda Ujumbe CECAFA
DC Bagamoyo awawashia moto waamuzi wa soka wa wilaya

Comments

comments