Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wananchi wanaoishi katika kata 19 zitakazofanya Uchaguzi mdogo wa Madiwani  kwa upande  Tanzania Bara na Ubunge katika jimbo la Dimani Zanzibar Januari 22, 2017 wajitokeze kwa wingi kupiga kura kuwachagua viongozi watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka 3.

Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa Semistocle Kaijage,alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  Mjini Zanzibar, amesema kuwa maandalizi ya Uchaguzi huo yamekamilika na amewataka wananchi wenye sifa za kupiga kura katika uchaguzi huo wajitokeze kutimiza wajibu wao kikatiba.

Kaijage amewapongeza wananchi wanaoishi katika Jimbo la Dimani,  Zanzibar na wale wa Kata 19 za Tanzania Bara zitakazofanya uchaguzi mdogo hapo kesho  kwa utulivu waliouonyesha wakati wa kipindi cha Kampeni za Uchaguzi.

“Licha ya kwamba kutakuwa na ulinzi wa kutosha katika vituo vya kupigia kura, Ni matumaini ya Tume kuwa hali ya Amani na Utulivu ambayo imekuwepo hadi sasa na kama ilivyokuwa katika Chaguzi zilizopita itaendelea kudumishwa ili kuhakikisha uchaguzi huu unafanyika kwa Utulivu, Amani na Ustawi wa Taifa letu” Amesema Jaji Kaijage.

Kwa upande wa Uchaguzi Mdogo wa Madiwani katika Kata 19 za Tanzania Bara Wapiga Kura 134,705 walioandikishwa wanatarajia kupiga kura  katika vituo 359 ambavyo vilitumika katika Uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

 

 

Video: Machinga Ilala waomba kurasmishwa, wamfananisha Rais Magufuli na...
#HapoKale