Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetoa tathmini  ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25,  2015,kwa kufanya mahojiano na halmashauri 75 hapa nchini, kujadiliana na wadau mbalimbali wa uchaguzi ili kupata mtazamo wao juu ya uchaguzi huo.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji. Damian Lubuva alipokuwa akikabidhi ripoti ya uchaguzi kwa ,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Jenista Muhagama kwa niaba ya Serikali, kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu Bungeni mjini Dodoma.

Lubuva amesema tathmini hiyo ina lengo la kujenga msingi bora wa kutekeleza chaguzi zijazo na kupata majibu ya changamoto zilizojitokeza kwenye Uchaguzi huo ikiwa ni pamoja na kujua kwa nini baadhi ya maeneo yalikuwa na mwitikio mdogo wa kupiga kura ikilinganishwa na wapiga kura waliojiandikisha.

“Matokeo ya tathmini hii pia yataisaidia Tume katika kujitathmini katika maeneo ya kiutendaji ikiwamo kurekebisha Sheria, Kanuni, masuala ya kisera na kufanya mapitio ya Mpango Mkakati wa Tume na Mkataba wa Huduma kwa Mteja” alisema Jaji Lubuva.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhani amesema takwimu za tathmini hiyo zimekusanywa kupitia mahojiano ya ana kwa ana kwa msaada wa madodoso na majadiliano ya makundi maalumu.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu  Jenista Muhagama amesema kuwa baada ya kupata matokeo ya tathmini, kwa kiasi kikubwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitekeleza majukumu yake ya Kikatiba kwa ufanisi mkubwa.

Lowassa aeleza kwanini hakuhudhuria misiba ya Sitta, Mungai
Video: Wajane wakimbilia Dar kutafuta maisha