Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imevitaka vyama vya siasa nchini kufuata sheria na kanuni za uchaguzi, zitakazo kuwa zinatolewa au kutangazwa na tume hiyo kwa lengo la kuendesha chaguzi za marudio zilizokuwa za haki na amani.

Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Tume hiyo, Dkt. Athumani Kihamia alipokuwa akitoa taarifa ya uchaguzi mdogo wa marudio wa Udiwani katika kata 21 za mikoa 10 ya Tanzania bara utakaofanyika Septemba 16 mwaka huu.

Amesema kuwa fomu za uteuzi wa wagombea wa uchaguzi huo zimepangwa kutolewa kati ya Agosti 17 na 23 mwaka huu, huku kampeni za uchaguzi zikipangwa kufanyika kati ya Agosti 24 hadi Septemba 15 mwaka huu.

“Tume inachukua fursa hii kuviasa vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani) za mwaka 2015,” amesema Dkt. Kihamia.

Aidha, uchaguzi huo mdogo wa udiwani katika kata 21 unatarajiwa kufanyika pamoja na uchaguzi mdogo wa Ubunge katika majimbo ya Korogwe Vijijini, Ukonga na Monduli na kata za Tindabuligi na Kisesa, katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu uliotangazwa siku za hivi karibuni ambao utakaofanyika siku ya Jumapili Septemba 16 mwaka huu.

Hata hivyo, Chaguzi hizo za marudio za udiwani na ubunge zinafanyika kwa lengo la kuziba nafasi zilizoachwa wazi na Madiwani na Wabunge waliohama vyama vyao kwa kujiuzulu, kufariki, na wengine kuvuliwa uanachama na viongozi wao.

 

Video: Inauma sana kumteua mpinzani- Msukuma
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Agosti 8, 2018