Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC) imewaonya wasimamizi wa uchaguzi ambao wataharibu au kukiuka taratibu za Uchaguzi kutokana na kutofuata sheria na taratibu zake.

Onyo hilo limetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salum Mbarouk wakati akifungua mafunzo kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi jijini Dodoma.

Amewataka wasimamizi hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea, ambapo amesema sheria ya taifa ya uchaguzi na ile ya serikali za mitaa zinaunda kosa la jinai na kutoa masharti ya adhabu kwa afisa yeyote wa uchaguzi ambaye atasababisha kuharibu uchaguzi.

“Madhara ya kutozingatiwa kwa taratibu za uchaguzi ni kusababisha kesi nyingi za uchaguzi na kuitumbukiza serikali katika gharama ambazo zingeweza kutumika katika shughuli nyingine za maendeleo”, amesema Jaji Mbarouk.

Kwa upande wake mkurugenzi wa uchaguzi Dkt. Athumani Kihamia amewataka washiriki wa mafunzo hayo kutoa ushirikiano kwa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mdogo ikiwa ni pamoja na kuvishirikisha katika kila hatua muhimu wakati wa mchakato wa Uchaguzi.

Jumla ya wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi 210 kutoka katika majimbo manne ya Serengeti, Simanjiro, Ukerewe na Babati Mjini pamoja na Kata 47 zinazotarajiwa kufanya uchaguzi mdogo Disemba 3, mwaka huu wanashiriki katika mafunzo hayo yatakayodumu kwa siku tatu jijini Dodoma

Video: CCM yazungumzia kutekwa Mo Dewji, Waziri ashusha rungu ajali magari serikalini
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Oktoba 25, 2018