Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imezindua rasmi programu ya utoaji wa Elimu endelevu ya mpiga kura nchini kwa kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana ya Songe iliyopo nje kidogo ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Uzinduzi wa programu hiyo ni kuanza rasmi kwa mkakati wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata elimu ya mpiga kura ili kujenga uelewa kuhusu majukumu ya Tume , utendaji wake  na uelewa wa chaguzi mbalimbali zinazofanyika nchini.

Akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo wakati wa uzinduzi wa program hiyo,Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Emmanuel Kawishe amesema kuwa NEC imeamua kuwafikia moja kwa moja wanachi ili iwapatie elimu kuhusu haki na wajibu walio nao kikatiba pia kuwajengea uelewa wa kutosha kuhusu taratibu zinazosimamia chaguzi nchini.

Amesema kuwa programu hiyo imezinduliwa kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu utendaji wa Tume na kazi za Tume ili kuongeza uelewa miongoni mwa jamii pia kuiwezesha Tume hiyo kupokea ushauri na maoni ya wananchi.

Bw. Kawishe ameeleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inalo jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura kwa mujibu wa Sheria kama ilivyoanishwa katika kifungu Na 4 (c) cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 na kuongeza kuwa imeanza kuwafikishia elimu ya mpiga wananchi kura moja kwa moja katika maeneo yao.

Aidha, amewaeleza wanafunzi hao kuwa ili mwananchi aweze kupiga kura  lazima awe amekidhi sifa na vigezo vilivyo ainishwa kisheria ikiwemo kutimiza umri wa miaka 18 na kuendelea, kupiga kura katika kituo alichojiandikishia kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi kifungu cha 63, kuwa na utimamu wa akili, kuwa na uraia wa Tanzania na vigezo vingine vilivyo ainishwa kisheria.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga kura Bi. Giveness Aswile akitoa ufafanuzi kuhusu wajibu wa Tume katika kushughulikia watu wenye mahitaji maalum hasa watu wenye ulemavu ambao wanaokidhi sifa za kupiga kura amesema kuwa Tume imekuwa ikiweka mazingira rafiki ya kuwawezesha kupiga kura.

“ Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika uchaguzi uliopita tuliweka mazingira mazuri kwa watu wenye ulemavu, na wale wasioona ambao wana uwezo wa kusoma na kuandika tukawawekea vifaa na karatasi maalum zenye nukta nundu ambazo zina majina ya wagombea wa vyama vyote ili kuwawezesha kupiga kura wao wenyewe bila msaada wa mtu yeyote” Amesisitiza Bi. Aswile.

Taasisi ya Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu yapewa siku 10 kulipa deni la sh. mil.100
Yanga, JKT Ruvu Sasa Kucheza Oktoba 26