Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Athumani Amasi ametangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba 14 hadi Desemba 1, 2022, Tanzania Bara na Visiwani, huku likiwafutia matokeo wanafunzi 333 kwa udanganyifu.

Amasi ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa habari hii leo Januari 29, 2023, na kuongeza kuwa kati ya watahiniwa hao waliofutiwa matokeo, mmoja ni wa maarifa (QT) na 332 watahiniwa wa shule.

Amesema, “Baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 333 kwa kufanya udanganyifu, kati yao mmoja ni mtahiniwa wa maarifa na 332 ni wa shule.” ambapo pia ametaja watahiniwa wengine waliofutiwa matokeo ni wanne ambao wameandika matusi katika mitihani yao.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) Athumani Amasi.

Amasi amesema vituo vitatu vimefungiwa kufanya mitihani baada ya kuthibitika kupanga na kufanya udanganyifu ambapoa amevitaja vituo hivyo ni Andrew Faza Memorial cha Kinondoni Dar es Salaam, Cornelius cha Kinondoni na Mnemonic Academy cha Halmashauri ya Mjini Magharibi visiwani Zanzibar.

Aidha amesema kati ya watahiniwa 520,558 wenye matokeo 456,975 sawa na asilimia 87.79 wamefaulu kwa kupata madaraja ya kwanza hadi la nne.

Amasi, ameeleza ufaulu huo umeongezeka kwa asilimia 0.49 kutoka wa mwaka jana ambapo watahiniwa 422,388 sawa na asilimia 87.30 walifaulu.

NECTA: Hakuna shule wala mwanafunzi bora
Tahadhari ya shambulizi: Serikali yaikosoa taarifa ya KLM