Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza tarehe rasmi ya kuanza kwa mitihani ya kujipima ya kidato cha pili ambapo limesema kuwa zaidi ya watahiniwa laki tano wa kidato cha pili kutoka shule za Sekondari 4725, Tanzania bara wanatarajiwa kuanza mitihani ya taifa ya upimaji wa kitaifa nchini.

Mitihani hiyo itaanza Novemba 12 hadi 23 2018, ambapo wavulana ni 261,159 sawa na asilimia 47.93 huku wasichana wakiwa 283,707 sawa na asilimia 52.07.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es salaam na Katibu Mtendaji wa Baraza la mitihani la taifa, Dkt. Charles Msonde alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa mwaka huu kumekuwa na ongezeko la watahiniwa 23,011 sawa na asilimia 4.41 ukilinganisha na mwaka 2017 ambao walikuwa 521,855.

“Mitihani ya kidato cha pili ni muhimu kwa wanafunzi na jamii kwakuwa tunapima uwezo na uelewa wa Wanafunzi katika yale waliyojifunza kwa miaka miwili,” amesema Dkt. Msonde.

Hata hivyo, Dkt. Msonde ameongeza kuwa tayari maandalizi yamekamilika ikiwemo usambazaji wa mitihani katika vituo vya mitihani.

Mwandishi wa habari afungwa miaka 12 jela
Moto waua makumi, 250,000 wakimbia makazi