Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF limeingia mkataba wa miaka miwili na kampuni ya Azam Media, wa haki za matangazo ya Kombe la shirikisho (ASFC) na michezo ya timu ya taifa.

Mikataba hiyo ya miaka miwili imesainiwa leo mchana katika hafla fupi iliyofanyika katika studio za Azam TV jijini Dar es salaam, ina jumla ya thamani ya shilingi bilioni 6.3.

Akizungumza kabla ya kusainiwa kwa mikataba hiyo mkurugenzi wa michezo wa Azam Media, Patrick Kahemele amesema  udhamini wa mashindano ya Kombe la FA ni wa miaka minne na utakuwa na thamani ya Shilingi 4.5 bilioni ambao utaanza msimu huu, baada ya ule wa mwanzo kumalizika.

Kahemele pia akaelezea kwa kina mkataba mwingine wa udhamini wa timu ya taifa, kwa kusema Azam Media itaipatia TFF kiasi cha Shilingi 100 milioni kwa mwaka kwa michezo ambayo haipo kwenye kalenda ya Shirikisho la soka duniani (FIFA) lakini pia kiasi cha Shilingi milioni 35 kwa kila mchezo.

“Tunaamini timu ya taifa ikipata idadi kubwa ya michezo ya kimataifa ya kirafiki, itatusaidia kupandisha kiwango cha ubora wa soka dunia,”

“Mataifa ya Afrika magharibi na kaskazini, yamekua yakitumia michezo hii kama sehemu ya kupandisha viwango vya ubora wa soka, tofauti na huku Afrika mashariki, Azam Media tumeona kuna umuhimu wa kuweka msisitizo kwa timu yetu ya taifa kupitia udhamini huu, ili na sisi tukuze kiwango chetu.” alisema Kahemele

Naye Rais wa TFF, Wallace Karia amesema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni ishara tosha ya nia ya dhati ya Azam Media katika kuendeleza soka nchini, ambalo siku za nyuma lilihitaji usaidizi wa kuwekeza kwa kiasi kikubwa.

“Mchakato wa kujadili mkataba huu yamepata baraka zote na umepia katika taratibu zote kama katiba ya TFF inavyotaka. Azam wamekuwa washirika wetu kwa asilimia 80 kwani wamekuwa wakitusaidia katika kusukuma mbele mipango yetu mingi ya kimaendeleo,” alisema Karia.

Kwa upande wa mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando amesema kuwa tangu kampuni hiyo ilipoanza kusapoti mchezo wa soka kumekuwa na maendeleo makubwa ya mpira wa miguu hapa Tanzania.

“Kumekuwa na ufanisi mkubwa kwa timu yetu ya taifa na pia tumeona ufanisi mkubwa kwa klabu zetu kwenye mashindano ya kimataifa.

“Azam Media tunaamini kwamba tuna mchango wetu katika kupatikana kwa ufanisi na mafanikio hayo,” alisema Mhando.

Katibu mkuu wa TFF Wilfred Kidao na waandishi wa habari nao walikua sehemu ya hafla hiyo ya kusaini mikataba.

Waitara: Chagueni wenyeviti wa mitaa wenye kipato (video)
JPM amteua Diwani kuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa