Kiungo Kutoka nchini Nigeria Nelson Esso Okwa ataendelea kuwa nje ya Kikosi cha Simba SC, kufuatia majeraha ya nyonga yanayomsumbua kwa muda sasa.

Okwa alisajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu huu 2022/23, akitokea kwa Mabingwa wa Soka nchini Nigeria Rivers United.

Kocha Juma Mgunda amethibitisha taarifa za majeraha ya Kiungo huyo alipozungumza Waandishi wa Habari leo Ijumaa (Novemba 18) majira ya mchana, kuhusu mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa kesho Jumamosi (Novemba 19).

Kocha Mgunda amesema Okwa amelazimika kuenguliwa kwenye kikosi kwa sasa, kufuatia majeraha ya nyonga yanayomsumbua kwa muda mrefu, hivyo hatoweza kumtumia kwa muda.

“Okwa yupo ila ni mgonjwa ana tatizo la nyonga na tatizo hilo kumbe alikuja nalo kutoka kwao na tumemruhusu aende akatibiwe.” amesema Kocha Mgunda

Wakati huo huo Mgunda amesema Kesho Jumamosi (Novemba 19) ataanza kumtumia Kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama, baada ya kumaliza adhabu ya kufungiwa michezo mitatu.

“Clatous Chama yupo na yuko fit na yuko tayari kucheza, inshallah kesho mnaweza mkamuona.” amesema

Chama alikosa michezo mitatu dhidi ya Singida United, Ihefu FC na Namungo FC kufuatia kosa la kushindwa kuwapa mkono wachezaji wa Young Africans, kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa Oktoba 23.

Watoto nane wafariki kwa surua Zanzibar
DART kuongeza wigo wa usafirishaji nchini