Kiungo kutoka nchini Nigeria Nelson Okwa amefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu hatma yake ndani ya Klabu ya Simba SC inayotajwa kufanya mabadiliko kwenye kikosi kwa kusajili wachezaji kadhaa wa kigeni wakati wa Dirisha Dogo.

Okwa alisajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu huu akitokea kwa Mabingwa wa Nigeria Rivers United FC, ambako alikua nahodha na kiungo wa kutegemewa kwenye kikosi cha klabu hiyo yenye Maskani yake mjini Port Harcourt.

Kiungo huyo amezungumza na Dar24 Media na kueleza kuwa bado ana Mkataba na Simba SC na hadi sasa hakuna mazungmzo yoyote yanayoendelea kuhusu kuvunjwa kwa mkataba wake.

Amesema yanayozungumzwa na kuandikwa katika Mitandao ya Kijamii kuhusu hatma yake ndani ya Klabu hiyo ya Msimbazi sio ya kweli, na kama ikitokea yataanikwa hadharani kwa sababu mchezo wa soka una tabia ya kuweka mambo wazi.

“Sifahamu lolote kuhusu kuondoka Simba SC, ninachojua mimi ni mchezaji halali wa klabu hii kwa mujibu wa mkataba uliopo kati yangu na Uongozi, ikitokea ninaondoka kila kitu kitafahamika.”

“Ninaona na kusoma mengi katika Mitandao ya kijamii kuhusu mimi, lakini bado ninasisitiza, Okwa ni mchezaji wa Simba SC na nitaendelea kuwa hapa kwa ajili ya kuipambania Simba SC kwenye Ligi ya ndani na Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.” amesema Okwa.

Okwa amekua na wakati mgumu wa kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza cha Simba SC, lakini sababu kubwa imekua ikitajwa ni majeraha, ambayo yalimuandama kwa zaidi ya mwezi mmoja, hadi kuepelekea kurudi kwao Nigeria kwa ajili ya kufanyiwa matibabu.

Mkwasa afunguka kilichomtoa Ruvu Shooting
Moses Phiri: Kiongozi wa Young Africans alinifuata Zambia