Ni jukumu la kila mdau kama vile serikali za Mitaa, wakulima, wafugaji, jumuia za watumiaji maji, watunzaji wa mazingira na taasisi binafsi kuhakikisha kwamba rasilimali maji zote zinalindwa kikamilifu kwa ajili ya uendelevu wa madakio ya maji na maisha kwa ujumla.   

Hayo  yamesemwa  na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mh.Reuben Mfune ambaye alikua Mgeni Rasmi wakati wa warsha ya  uzinduzi wa Mradi wa utafiti wa usimamizi endelevu wa madakio ya maji kupitia tathimini ya kuimarisha mtiririko wa maji kwa mazingira na utekelezaji wake katika kulinda Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi kutokana na athari za shughuli za kibinadamu , Tanzani(EFLOWS) . Uzinduzi huo umefanyika Rujewa-Wilayani Mbarali katika Mkoa wa Mbeya.

Vilevile Mheshimiwa Mfune,  ametoa  shukrani kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhifadhi wa Mazingira (UNEP) kwa ufadhili wa kifedha katika mradi huo, pia Sekretarieti ya Azimio la Nairobi (Nairobi Convection Secretariat) ambayo ni msimamizi wa utekelezaji. Pamoja  na Waratibu wa mradi huo kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kujitoa kwao kutekeleza mradi huu ambao ni mojawapo ya miradi iliyopo katika nchi zilizo kwenye Mpango Mkakati wa nchi za Magharibi mwa Ukanda wa Bahari ya Hindi.

Aidha, amesema kuwa anafurahi  kuona kwamba masuala ya mazingira kama vile umwagiliaji, kilimo kandokando ya kingo za mito, ufugaji wa mifugo ndani ya kidakio cha mto Mbarali na Bonde la Rufiji pamoja na ongezeko la watu, vinasimamiwa kwa uhifadhi kamilifu wa eneo la Magharibi mwa Ukanda wa Bahari ya Hindi. Na muhimu zaidi kwa ajili ya mtiririko endelevu wa maji kuelekea Mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere (Julius Nyerere Hydro Power Project  – JNHPP).

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC katika hotuba yake  ya ukaribisho kwa mgeni Rasmi iliyosomwa kwa niaba yake na Meneja wa Utafiti-NEMC Bi Rose Salema Mtui amesema kuwa  NEMC kwa kushirikiana na taasisi za kitaaluma/utafiti zimekuwa zikitengeneza miradi/programu  na kufanya tafiti na mojawapo ni kama mradi huo uliozinduliwa kwa lengo la kutatua matatizo mbalimbali ya kimazingira. 

“Kupitia mradi huu, utekelezaji wa mtiririko wa maji kwa mazingira (env. flow) ni muhimu sana kwa uendelevu wa ikolojia ya mto; na natumaini wadau wote na Serikali kwa ujumla watakuwa tayari kutoa ushirikiano mkubwa kuhakikisha malengo ya mradi huu yametimia” alisema.

Akiongea katika warsha hiyo ya Uzinduzi Mkurugenzi wa Shahada za Juu Uhawilishwaji wa teknolojia za Kitafiti kutoka Chuo Cha Sokoine SUA Profesa Ezron Karimuribo  amesema kuwa kuna uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji Nchini na umetokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu kama vile ukataji miti, uchomaji misitu, kilimo pembezoni mwa vyanzo vya maji, uchimbaji madini,ufuagji na uchepushaji wa maji. Hivyo basi katika mradi huo  ambao utafanyika katika wilaya ya Mbarali  na wilaya hiyo imechukuliwa kama kianzio tu.

Mradi huo utafiti wa usimamizi endelevu wa madakio ya maji kupitia tathimini ya kuimarisha mtiririko wa maji kwa mazingira na utekelezaji wake katika kulinda Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi kutokana na athari za shughuli za kibinadamu , Tanzani(EFLOWS unaratibiwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA).

DKT Hussein Mwinyi atoa maelekezo kwa Wizara ya mambo ya nje
Rais Samia kupokea ndege mpya ya 9 kesho