Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira – NEMC, pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kuongeza nguvu zaidi katika kusimamia utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini.

Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo mara baada ya kuongoza zoezi la kufanya usafi katika soko kuu la wamachinga mjini Dodoma ikiwa ni katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani leo tarehe 5 Juni 2023 na kuongeza kuwa ni lazima kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa kwa wanaokiuka maagizo hayo.

Ameongeza kuwa, ni vyema kuhakikisha mifuko yote inayozalishwa inaonesha taarifa za mzalishaji na kama inakidhi viwango vilivyowekwa na mamlaka husika. Pia amesisitiza makampuni na watu binafsi wanaozalisha bidhaa za plastiki kuhakikisha taka zinazotokana na bidhaa zinazozalishwa zinakusanywa na kuondolewa.

Halikadhalika Makamu wa Rais amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kampuni zinazopewa kazi ya kuzoa taka ziwe na uwezo kufanya kazi hizo kwa ufanisi na kukemea utoaji wa tenda za uzoaji taka kwa kampuni zisizokuwa na uwezo na zile zisizo na vitendea kazi vya kisasa.

Orebonye: Young Africans ilistahili ubingwa
Fiston Mayele: Hatukuwa na bahati ya ubingwa