Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limefunga machinjio madogo ya Msalato Jijini Dodoma kwa muda usiojulikana pamoja na kutoza faini ya shilingi milioni 5 kwa kosa la kukithiri kwa uchafu na miundombinu chakavu.

Hatua hiyo imefikiwa mara baada ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kufanya ziara ya kushtukiza katika eneo hilo na kujionea mazingira yasiyoridhisha kwa usalama wa afya za binadamu.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Mussa Sima amesema lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya hali hiyo kwa manufaa ya afya za walaji na kwamba ziara za namna hiyo zitaendelea kwa maeneo mengine ili kubaini hali halisi na kuchukua hatua.

“Kwa sisi watu wa mazingira kiukweli afya za binadamu ni kipaumbele namba moja, hali hii haikubaliki na ni lazima hatua stahiki zichukuliwe ili kukomesha hali hiyo,” amesisitiza Sima.

Katika ziara hiyo wabunge wamejionea mazingira hatarishi kwa afya za watumiaji wa nyama inayochinjwa machinjioni hapo ikiwa ni pamoja na kurundikana kwa samadi, kukithiri kwa harufu kali na kukosekana kwa maji safi.

Kufuatia hali hiyo Naibu Waziri Sima amemuagiza Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Nchini (NEMC) Dkt. Samwel Gwamaka kufanya tathmini ya kina na kuhakikisha machinjio yanazingatia taratibu zilizopo katika sheria ya mazingira ya mwaka 2004.

“Mkurugenzi wa NEMC fanya tathmini ya uhakika na ya kina kihakikisha machinjio yanazingatia taratibu kwa mujibu wa sheria za nchi hasa ile ya mazingira ya mwaka 2004 lazima tulinde afya za wananchi,” ameongeza Naibu Waziri Sima.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira Kanali Mstaafu Masoud Ali amesema hali ya usafi katika machinjio hiyo haidhirishi ni sahihi NEMC kuchukua hatua.

“Kiukweli NEMC msingechukua hatua, sisi kamati tungechukua maana haiwezekani hali hii ambayo ni hatari kwa afya ikavumiliwa na ni wazi kuwa haikubaliki na yeyote,” amesisitiza Ali.

Awali Afisa Mifugo wa Jiji la Dodoma Gratius Mwesiga ameieleza Kamati hiyo kuwa ukarabati wa eneo hilo umeanza na unaendelea kwa awamu ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa mifumo ya maji taka.

Kwa mujibu wa kifungu namba 194 cha sheria ya usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, faini hiyo iliyotozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) inatakiwa kulipwa ndani ya wiki mbili.

Video: Jurgen klopp azua balaa Uingereza, agoma kuipeleka Liverpool uwanjani
Chukua haya unapomtembelea mama aliyejifungua, ''Using'ang'anie kubeba mtoto''