Mwanasheria wa Baraza la Mazingira la Taifa la NEMC, Manchare Heche amesema kuwa uwepo wa mifuko ya plastiki husababisha vifo vya viumbe hai zaidi ya laki moja vilivyopo baharini kutokana na mifuko hiyo kuchukua muda mrefu kuharibika.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo zimebaki siku 2 tu kuelekea marufuku ya mifuko ya plastiki inayotarajiwa kuanza Juni Mosi 2019.

“Tuangalie pia faida tunayoipata kama nchi, mifuko hii tunayoiondoa inaweza kukaa miaka 500, kwa hiyo kadri inavyoingia mtaani inahatarisha maisha ya watu, mfano sekta ya uvuvi huku zaidi ya viumbe laki moja hufariki sababu ya mifuko ya plastiki.”amesema Heche

Aidha, amesema kuwa mikoa ambayo inategemea uvuvi ikipoteza viumbe laki moja kwa mwaka ni hasara kubwa, huku takwimu za UNEPO zinaonyesha kuwa mpaka kufika 2050 kutakuwa na mifuko mingi kuliko Samaki.

Kuhusiana na gharama kuongezeka za mifuko mbadala Manchare Heche amesema kuwa Serikali kazi yake kubwa ni kuweka mazingira mazuri ya watu ya kufanya biashara, akisema kuwa mpaka sasa kuna viwanda zaidi ya 70, vimeshaingia kwenye soko la mifuko mbadala, hiyo yote ni serikali kuhamasisha ili mifuko bei yake iweze kushuka.

Hata hivyo, kuanzia Juni Mosi 2019, Serikali itaanza utumiaji wa kanuni zinazopiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki.

UVCCM Iringa waaswa kuwatetea wanachama
Matokeo chanya Sekta ya Madini tumeanza kuyaona- Dkt. Abbasi