Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli amelitangazia taifa usiku wa kuamkia leo kifo cha aliyekuwa raisi wa Tanzania mzee wetu Benjamin William Mkapa.

Hakika hii ni huzuni kwa kila Mtanzania na mzalendo lakini kwa sisi watu wa soka mzee Mkapa atadumu mioyoni mwetu kila tukiutazama urithi alitouachia wa UWANJA WA TAIFA WA KISASA.

Wazo la uwanja huu wenye uwezo wa kuingiza watu 60,000 lilikuja katika awamu yake na mwaka 2005 uwanja huu ulianza kutengenezwa na kufunguliwa 2007 ikiwa moja ya viwanja bora sana barani Afrika.

Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Julai 24, 2020 jijini Dar es Salaam alipokuwa anapatiwa matibabu katika hospitali jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ya Tanzania ikimnukuu Rais John Magufuli imeeleza kuwa Rais mstaafu Mkapa alikuwa amelazwa jijini hapa.

Kufuatia kifo cha Rais huyo mstaafu, Rais Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo ambapo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

“Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa, Mzee wetu Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu amefariki dunia katika hospitali jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa, niwaombe Watanzania tulipokee hili, tumepata msiba mkubwa tuendelee kumuombea mzee wetu ambaye ametangulia mbele za haki,” amesema Rais Magufuli

Pia Rais Magufuli amewataka Watanzania kuwa wastahimilivu baada ya kupokea taarifa za msiba huo mzito.

Rais mstaafu Mkapa alizaliwa Novemba 1938 wilayani Masasi mkoani Mtwara, ambapo aliiongoza nchi kwa awamu mbili kuanzia mwaka 1995-2005.

Kiongozi huyo atakumbukwa kwa utumishi wake na hata baada ya kustaafu aliandaa kitabu kilichoangazia mambo mbalimbali ya maisha yake.

PUMZIKA KWA AMANI (RIP) BENJAMIN WILLIAM MKAPA, NA ASANTE KWA ULIYOTUFANYIA.

Katwila aahidi kujiuzulu Mtibwa Sugar
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Julai 24, 2020