Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil, Neymar da Silva amesema kuwa kipigo cha 2-1 dhidi ya Ubelgiji kilichosababisha kuondolewa kwenye fainali za kombe la dunia katika hatua ya robo fainali kimemuachia huzuni ambayo hajawahi kuipata katika maisha yake yote ya soka.

Nyota huyo wa klabu ya Paris St Germain amesema kuwa kipigo hicho kimemsababisha kuwa na wakati mgumu kurejea kwenye klabu yake, lakini hana budi kupiga moyo konde.

“Ninaweza kusema ni kipindi cha masikitiko/huzuni kubwa zaidi katika maisha yangu ya Soka, maumivu ni makubwa kwa sababu tunajua tungeweza kufika mbali na tulijua tuna uwezo wa kufika mbali na kutengeneza historia, lakini haikuwa muda huu,” aliandika kwenye Instagram.

“Ni ngumu kupata nguvu ya kutaka kurejea kwenye klabu yangu tena lakini nina imani Mungu atanipa ujasiri kuyakabili yaliyo mbele yangu,” aliongeza.

Hata hivyo, alifafanua kuwa ana furahi kushirikiana na timu yake ya Brazili anayoipenda na kujivunia. Alisema kuwa Ubelgiji wameingilia ndoto yao lakini hawakuiondoa kwenye akili na mioyo yao.

Brazil walipokea kipigo cha 2-1 katika mchezo uliofanyika Kazan, Ijumaa iliyopita na kuwaondoa kwenye mategemeo ya wengi kuwa ingeweza kushinda Kombe la Dunia kwa mara ya sita.

Goli pekee la Brazil lilifungwa na Renato Augusto (dakika ya 76), Fernandinho alijifunga katika dakika ya 13 na kuwapa Ubelgiji goli la kwanza. Ubelgiji waliongeza goli la pili katika dakika ya 31 kupitia kwa Kevin De Bruyne.

Watoto nane kati ya 12 waokolewa wakiwa hai Thailand
Mgogoro wa Madaraka wazalisha Makamu wanne wa Rais