Mchezaji wa Brazil Neymar anatarajiwa kutoa ushahidi katika mahakama moja ya Hispania kuhusu madai ya ufisadi yanayozunguka uhamisho wake katika klabu ya Barcelona.

Aliyekuwa rais wa kilabu hiyo pamoja na yule wa sasa wamekana kufanya makosa yoyote katika uhamisho huo wa mchezaji huyo.

Barcelona inasema ililipa Euro milioni 57 kwa ununuzi wa Neymar mwaka 2013, huku wazazi wake wakipokea Euro milioni 40 na kilabu ya Santos ikipokea Euro milioni 17.

Lakini uchunguzi unasema kuwa ada hiyo ilikuwa karibu Euro milioni 83 na Barcelona ilificha kiasi kikubwa cha pesa kwa kuandika tofauti kwenye mkataba wa Neymar.

Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani na kampuni ya uwekezaji ya DIS ambayo ilimiliki asilimia 40 ya haki za michezo za nyota huyo.

DIS inadai kwamba iliathiriwa kifedha na uhamisho huo ilipopokea Euro 6.8 za Euro milioni 17 zilizolipwa kilabu ya Santos na kwamba ilinyimwa haki yake.

Rais wa kilabu ya Barcelona, Josep Maria Bartomeu na mtangulizi wake Sandro Rosell walifikishwa mahakamani mjini Madrid siku ya Jumatatu,wakisisitiza kuwa hawakukiuka sheria zozote.

Baba na mama mzazi wa Neymar pia walitarajiwa kufika katika mahakama hiyo ya kitaifa mjini Madrid.

Azam FC Kuzileta Dar es salaam Zesco, Zanaco
Floyd Mayweather Atoboa Siri Ya Ushawishi Wa Pesa