Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil Neymar da Silva Santos Júnior, amesema bado hajawa fit kwa asilimia 100, kufuatia upasuaji aliofanyiwa baada ya kuumia mguu wake wa kulia akiwa kwenye majukumu ya kuitumikia klabu ya PSG nchini Ufaransa.

Neymar amesema, bado anaendelea kufanya mazoezi ambayo yatamuwezesha kuwa fit kwa kiwango kinachotakiwa, na ana matumaini hatua hiyo ataifanya ndani ya muda, kabla ya kwenda nchini Urusi kushiriki fainali za kombe la dunia akiwa na timu ya taifa lake la Brazil.

Mshambuliaji huyo hakuwahi kucheza soka tangu alipoumia mwezi Februari wakati wa mchezo wa ligi ya Ufaransa dhidi ya Olympic Marseille, lakini mazoezi aliyokua akiyafanya chini ya uangalizi wa madaktari wa klabu yake, yalimuwezesha kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa siku kumi zilizopita.

Neymar amesema: “Sijawa fit kwa asilimia 100. Lakini nina uhakika nitafanikiwa kwa wakati. Bado ninahofia kufanya baadhi ya mambo ninapokua katika mazoezi yangu, japo kuna baadhi ya vitendo nimeanza kujaribu na ninafanikiwa.

“Itachukua muda wa siku kadhaa kabla ya kwenda kushiriki fainali za kombe la dunia nikiwa na timu yangu ya taifa, nina uhakika muda utakapokua tayari nitakua na uwezo wa kucheza soka vizuri.”

Neymar alisema maneno hayo saa chache kabla ya kupanda ndege na kuelekea mjini London nchini England, ambapo kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kimeweka kambi ya kujiandaa na fainali za kombe la dunia.

kama itakumbukwa vyema Neymar mwenye umri wa miaka 26, alikua na bahati mbaya ya kuumia akiwa katika fainali za kombe la dunia 2014, katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Colombia, jambo ambalo lilimnyima nafasi ya kucheza kwenye mpambano wa nusu fainali uliomalizika kwa Brazil kuchapwa mabao saba kwa moja dhidi ya Ujerumani.

Kikosi cha Brazil kinatarajia kucheza michezo miwili ya kujipima nguvu dhidi ya Croatia kwenye uwanja wa Anfield Juni 3 na baadae kitacheza dhidi ya Austria mjini  Vienna Juni 10, na kisha kitaanza safari ya kuelekea Urusi.

Mabingwa hao wa dunia wa kihistoria wamepangwa katika kundi E, na wataanza kampeni ya kusaka ubingwa wa 2018 kwa kucheza dhidi ya Uswiz Juni 17 kwenye uwanja wa Rostov-on-Donand, kisha watapapatuana na Costa Rica Juni 22, katika uwanja wa Saint Petersburg na watamaliza michezo ya hatua ya makundi dhidi ya Serbia mjini Moscow Juni 27.

Jamie Maclaren aitwa kuchukua nafasi ya Tomi Juric
Fahamu dalili 14 za kisukari, chukua hatua