Mabingwa wa soka nchini Italia, Juventus wameandaa ofa ya Pauni milioni 25, kwa ajili ya usajili wa kiungo kutoka nchini Ufaransa na klabu ya Leicester City, N’Golo Kanté.

Juventus wanajiandaa kufanya usajiali wa kiungo huyo, kutokana na kuridhishwa na uwezo wake mkubwa wa kucheza soka aliouonyesha msimu uliopita, na kuisaidia klabu ya Leicester City kutwaa ubingwa wa England.

Baadhi ya maafisa waliopendekeza suala la usajili wa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25, wanaamini Kanté anaweza kufanikisha baadhi ya mipango ya klabu ya Juventus kuelekea msimu wa 2016-17, ambao umepangwa kuanza kuunguruma mwezi August mwaka huu.

Hata hivyo baadhi ya wadadisi wa soka nchini Italia, wameeleza kwamba huenda usajili wa Kanté unataka kufanywa klabuni hapo, kwa lengo la kutaka kuziba nafasi ya kiungo Claudio Marchisio, ambaye anaendelea kuuguza majeraha hadi mwezi Novemba mwaka huu.

Wakati mipango hiyo ikipangwa huko mjini Turin nchini Italia, mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid, nao wamedhamiria kumsajili Kanté, hivyo huenda ushindani ukawa mkubwa.

Kwa sasa Kante yupo nchini Ufaransa akiwa na timu yake ya taifa inayoshiriki fainali za Euro 2016.

Wanawake Zaidi Kufanya Maamuzi ya Kura katika Tuzo za Oscar
18 Wafariki kwa Kulipukiwa na Bomu Somalia