Uongozi wa klabu ya Chelsea unajipanga kumsainisha mkataba mpya kiungo kutoka nchini Ufaransa N’Golo Kante, ambao utamuwezesha kuwa mchezaji anaelipwa mshahara mkubwa klabuni hapo.

Chelsea wanajipanga kufanya hivyo, ili kuzima ndoto za mabingwa wa soka nchini Ufaransa PSG, ambao wanatajwa kuwa kwenye mawindo makali ya kuisaka saini ya kiungo huyo, ambaye anaendelea kuwika kwenye ligi ya nchini England.

PSG walianza kutajwa kumuhitaji Kante mara baada ya fainali za kombe la dunia, ambapo kiungo huyo alionyesha uwezo mkubwa akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa na kusaidia kufanikisha lengo la kutwaa ubingwa wa fainali hizo zilizounguruma nchini Urusi.

Taarifa kutoka jijini London zinaeleza kuwa, mkataba mpya unaoandaliwa kwa ajili ya Ngolo Kante, utamuwezesha kulipwa mshahara wa Pauni 290,000 kwa juma, na inaaminika ni sehemu ya kumshawishi kusalia klabuni hapo.

Hata hivyo bado haijafahamika ni lini Kante na uongozi wa Chelsea watakaa meza moja na kukamilisha dili la kusaini mkataba huo mpya.

Kwa sasa mchezaji ambaye anaelipwa mshahara mkubwa kwenye klabu ya Chelsea ni kiungo mshambuliaji Eden Hazard.

Mshahara wa kiungo huyo kutoka nchini Ubelgiji unatajwa kufikia Pauni milioni saba kwa mwaka, na endapo Kante atasaini mkataba mpya atakua akilipwa mshahara wa Pauni milioni kumi na moja kwa mwaka.

Msimu huu wa 2018/19 ni watatu kwa Kante kuitumikia Chelsea tangu aliposajiliwa akitokea    Leicester City kwa ada ya Pauni milioni 32.

Tayari ameshatwaa ubingwa wa England mara mbili, msimu wa 2015/16 akiwa na Leicester City na msimu wa 2016/17 akiwa na Chelsea.

Pia ametwaa ubingwa wa kombe la FA mara moja akiwa na The Blues mwishoni mwa msimu wa 2017/18.

USSF wampigia hesabu Julen Lopetegui
Arsenal kusaka mshambuliaji Januari 2019

Comments

comments