Timu ya Taifa ya Tanzania Bara kwa umri chini ya miaka 20, hii leo imeondoka mjini Jinja kuelekea mji wa Gulu, umbali wa zaidi ya kilomita 400 kwaajili ya mchezo wa robo fainali dhidi ya Uganda siku ya Jumapili.

Tanzania Bara iliyomaliza kama vinara wa kundi B la michuano ya CECAFA U20 Chalenji Cup inayoendelea nchini hapa, inakutana na Uganda iliyoshika nafasi ya tatu katika kundi A.

Mkuu wa msafara wa timu hiyo, Khaleed Mohammed amesema hali ya wachezaji wote iko vizuri kuelekea kwenye mechi hiyo, isipokuwa golikipa Ally Salim aliyepata majeraha kwenye mechi dhidi ya Kenya.

“Timu imeondoka hapa Jinja leo asubuhi kwenda Gulu ikiwa kwenye hali nzuri kabisa. Lengo letu ni kufanya vizuri kuhakikisha tunakwenda mbele zaidi ikiwezekana kuondoka na kombe,” alisema Mohammed.

“Kwa kifupi mipango yote iko vizuri. Kama viongozi tunahakikisha wachezaji wetu wanapata kila wanachohitaji ili waweze kushindana,” alisisitiza.

Timu hiyo ya Tanzania Bara imeonyesha uwezo mkubwa katika mashindano hayo ikizifunga timu za Ethiopia mabao 4-0 na Zanzibar 5-0, huku ikilazimishwa sare ya mabao 2-2 na Kenya.

Mechi za robo fainali zitachezwa siku ya Jumapili na Jumatatu kwenye miji ya Jinja na Gulu. Mechi nyingine za robo fainali ni Eritrea na Zanzibar, Sudan Kusini na Sudan Kaskazini huku Kenya ikicheza na Burundi.

IMEANDALIWA NA GIFT MACHA
AFISA HABARI TANZANIA BARA U20
CECAFA U20 UGANDA 2019

Je unatafuta kazi? hapa nafasi mbalimbali za kazi zimetangazwa
Daktari awashauri wanaume kulia, 'msihofie kuchekwa'