Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Serikali haitazifumbia macho NGO’s zote zinazojiingiza katika masuala yanayohatarisha usalama wa Nchi au kujiingiza katika vitendo visivyofaa kama utakatishaji fedha na ugaidi.

Ameyasema hayo wakati wa hotuba yake alipokuwa akifungua Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali uliondaliwa na Baraza la Taifa la NGO’s mapema Jijini Dodoma ambapo ameyataka Mashirika hayo kuepuka vitendo vya udanganyifu.

Ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali kuzingatia vipaumbele vya Taifa ili kuepukana na changamoto ya mashirika mengi kufanya kazi katika eneo moja jambo ambalo linaacha maswali kwa kuwa Tanzania ni moja kwa nini mashirika mengi yanajielekeza na kutoa huduma sehemu fulani ya Nchi wakati kuna maeneo mengine ya kipaumbele yanakuwa hayana mdau wa NGO’s hata moja.

Aidha, ameongeza kuwa NGO’s zote nchini zinatakiwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali na kuacha tabia ya baadhi ya NGO’s zinazoitaka Serikali kufuata matakwa ya NGOs hizo katika suala zima la mahali zinapotaka kufanya kazi.

Katika hotuba yake kwa Wajumbe wa Mkutano huo Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa kwa sasa Serikali imekamilisha kanzidata ya NGOs zote Nchini lakini pia kuweka mfumo wa kielektroniki ili kuhakikisha taarifa zote za NGOS zinafika kwa wakati.

Pia Ndugulile amezitaka NGOs kote Nchini kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji kama ambavyo NGOs zimekuwa zikiitaka Serikali kutekeleza wajibu huo na kuziagiza kuhakikisha zinatangaza na kuweka wazi kiasi cha fedha wanazopata kutoka kwa wafadhili wao ili jamii na Serikali wajue matumizi ya fedha hizo lengo likiwa ni kushirikiana baina ya Serikali, wanufaika na Mashirika hayo.

Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali unaendelea Jijini Dodoma ambapo Naibu Waziri Ndugulile amewaambia Wajumbe wa Mkutano huo kuwa Serikali inaendelea kuboresha Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kutumia fursa hiyo kuwambia wajumbe hao kuhusu kukamilika kwa uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Mshirika hayo Dkt. Richard  Faustine Sambaiga.

Masharti ya Ariana Grande yawachefua waandishi, watishia kumsusia
Video: Spika Ndugai alitekeleza sheria- Wakili Manyama