Rais Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, ameshinda tena kuiongoza nchi hiyo katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ambapo Tume ya Uchaguzi imesema kuwa ameseshinda kwa asilimia 94.9 ya kura zote zilizopigwa huku idadi ya waliopiga kura iikiwa ni asilimia 98 ya raia wote walioandikishwa.

Obiang, mwenye umri wa miaka 80, aliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi ya jeshi ya mnamo mwaka 1979, hivi sasa Nguema ndiye kiongozi aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi ukiondoa orodha ya watawala wa kifalme.

Mkuu wa tume ya uchaguzi nchini Guinea ya Ikweta Faustino Ndong Esono Eyang alithibitisha kuwa Obiang ataendelea na wadhifa wa urais kwa muhula mwingine wa miaka saba.

Katika uchaguzi wa mwaka huu uliofanyika Jumapili iliyopita, Nguema alikuwa akiungwa mkono na muungano wa vyama vya siasa 15 ikiwemo chama chake cha PDGE.

Chama hicho ambacho ndiyo kilikuwa taasisi halali ya kisiasa nchini Guinea ya Ikweta hadi mwaka 1991, kimeshinda pia viti vyote vya Bunge la Taifa na Baraza la Seneti.

Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Guinea ya Ikweta

Hata hivyo tume ya uchaguzi haikutangaza asilimia ya matokeo waliyopata wagombea wa urais wa upande wa upinzani ambao ni Andres Esono Ondo wa chama cha Convergence for Social Democracy na Buenaventura Monsuy Asumu wa chama cha Social Democratic Coalition Party.

Kabla ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi vikosi vya usalama viliwakamata wanasiasa kadhaa wa upinzani chini ya kile utawala wa nchi hiyo ulikitaja kuwa kuzima njama za kufanyika mashambulizi kwenye mji mkuu Malabo na katika mji mkubwa wa kibiashara wa Bata.

Serikali pia iliifunga mipaka yake ya ardhini na mataifa jirani ya Gabon na Cameroon kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi, ikisema inazuia wahujumu kutovuruga uchaguzi.

Obiang ni rais wa pili wa Guinea ya Ikweta tangu taifa hilo lipopopata uhuru mwaka 1968 kutoka Uhispania, iliyokuwa mtawala wake wa kikoloni kwa karibu karne mbili. Licha ya utajiri mkubwa wa mafuta, taifa analoongoza linaorodheshwa kuwa miongoni mwa yale masikini zaidi duniani.

Rushwa na ufujaji wa mali ya umma ni masuala yanayotajwa kukita mizizi ndani ya utawala wa miongo minne wa familia ya Nguema.

RC Makalla amewata wananchi kuendelea kupata chanjo ya Uviko-19
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Novemba 27, 2022