Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametangaza kuwa siku ya Jumamosi, Juni 22 ni siku ya maombi kwa mkoa wake kwaajili ya kuiombea Taifa Stars.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, mkutano uliohudhuriwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe.

Amesema kuwa siku ya jumamosi Juni 22, 2019 itakuwa ni siku ya maombi ya mkoa wa Dar es salaam kuiombea timu ya Taifa, Taifa Stars, hivyo amewaomba wananchi kuungana na wanamichezo wote kuiombea timu kwasababu jumapili inacheza na Senegal.

”Moja ya jambo ambalo mimi naliamini ni maombi, naomba mpenzi na mkereketwa wa michezo Jumamosi tuungane kwenye ulimwengu wa roho kuiombea Stars. Maandalizi yapo, nguvu ya pesa ipo lakini mkono wa Mungu hauepukiki kwenye ushindi, wengine huita bahati lakini tukimuomba Mungu atatupa majibu sahihi kwamba Tanzania itapata mafanikio makubwa,” amesema Makonda.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amezindua kampeni ya kuichangia Taifa Stars ambayo amesema itaendelea hadi Alhamisi, Juni 20, ambapo itafanyika hafla maalumu itakayohudhuriwa na viongozi wa serikali.

Halmashauri ya Njombe yatekeleza agizo la Serikali kwa Wanawake
Alikiba afanya mazungumzo na balozi wa Ufaransa