IKIWA ni saa kadhaa tu baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Ruvu Shooting jumapili iliyopita, kikosi cha Mbeya City fc kipo mkoani Mtwara kwa ajili ya ‘kupepetana’ na Ndanda Fc katika mchezo mwingine wa ligi kuu ya Soka Tanzania Bara hapo kesho.

Muda mfupi uliopita kocha mkuu wa City, Kinnah Phiri, ameidokeza mbeyacityfc.com kuwa amewandaa vijana wake kupambana kwa ‘jihad’ kuhakikisha wanashinda mchezo huo kujaribu kupunguza presha iliyopo kikosini hasa baada ya matokeo mabaya kwenye michezo miwili iliyopita.

“Tumepoteza mara mbili, hakika tumekuwa na presha kubwa, kitu muhimu kwetu ni kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha tunaondosha hali iliyopo kwa kushinda mchezo, hatuna shida kikosini kwa sababu wachezaji wetu safi  na waliokuwa majeruhi wamerudi ikiwa ni pamoja na golikipa wetu namba moja,hivyo kwa mchezo dhidi ya Ndanda hapo kesho timu iko ‘fiti’ na tayari kwa mchezo alisema.

Kuhusu kupoteza mchezo uliopita  Kocha  Phiri alitupa lawama kwa waamuzi wa soka nchini kuwa wamekuwa sehemu ya timu kadhaa kupoteza mchezo hata kama zilikuwa na uwezo wa kuweka matokeo sawa pale zinapokuwa tayari zishafungwa bao la mapema.

“kwenye soka la Tanzania tatizo kubwa la kwanza ni waamuzi, mara kadhaa wamekuwa wanashindwa kuchezesha kwa  kufuata sheria za mchezo wa soka, hili huleta matokeo kwa timu zisizostahili, kwenye mchezo ule tuliona jinsi gani vijana wetu walivyocheza vizuri hata baada ya kufungwa bao, tulikuwa na nafasi ya kurudisha na kushinda lakini mwamuzi hakuwa sawa,alishindwa kutenda haki hata kwenye tukio la wazi ambalo tulitakiwa kupewa penati lakini hakutoa”alisema.

Akiendelea zaidi kocha Phiri alisema  hafikirii tena juu ya yaliyopita anatizama mbele  kuhakikisha timu inafanikiwa zaidi kwenye michezo ijayo na kuwataka mashabiki wa City kutulia na kuwa na imani na timu yao kwa sababu bado iko safi  kuna wakati kukosa matokeo kunaletwa na mambo mengi ikiwemo hali ya miuondo mbinu ya nchi.

“Wito wangu kwa mashabiki watulie wawe na imani na timu na kuendelea  kuisapoti kwa sababu bado iko kwenye hali nzuri,mara kadhaa  uchovu wa safari ndefu  unawafanya wachezaji kushundwa kucheza kwenye kiwango chao jambo linalochangia  kupoteza mchezo,ninawaahidi kuwa timu itarudi kwenye ubora wake na kucheza vizuri kuhakikisha tunapata matokeo kwenye michezo mingi ijayo” alimaliza.

Kichunya Mchezaji Bora Septemba VPL
Mbowe abwagwa Mahakamani, atakiwa kulipa sh. bil. 1.7 kurudishiwa vitu vyake