Ligi kuu soka nchini Uingereza itaendelea tena usiku wa leo kwa mchezo mmoja mkali kati ya Leicester City dhidi ya Manchester City.

Mtanange huo utapigwa nyumbani kwa Leicester kunako dimba la King Power huku wenyeji hao wakiwa wanashika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 38 wakati Man City wakiwa nafasi ya nne na pointi zao 35.

YUPI ANACHEZA NA YUPI HACHEZI?

Wapachika mabao wawili wa Leicester Jamie Vardy naRiyad Mahrez ambao Jumamosi walifanyiwa mabadiliko kwenye dimba la Anfield, usiku wa leo watakuwa tayari kushuka dimbani.

Naye Danny Drinkwater atakuwa tayari kurejea dimbani.

Nahodha wa Manchester City Vincent Kompany huenda asicheze leo baada ya kupatwa na jeraha la shingo kwenye mchezo dhidi ya Sunderland.

Mshambuliaji Sergio Aguero leo atarejea dimbani lakini Pablo Zabaleta na Fernando huenda wasicheze.

MAKOCHA WANASEMAJE?

Kocha mkuu wa Manchester City, Manuel Pellegrini anasema ni lazima waichukulie Leicester kama timu yenye uwezo wa kupigania taji la ubingwa hadi mwisho wa msimu.

Amesema walikuwa kileleni mwa ligi na wanastahili kuwepo mahali hapo.

Naye kocha mkuu wa Leicester, Claudio Ranieri amesema kitendo cha kukumbana na Man City ni mtihani mwingine mkubwa lakini lengo lake ni kushinda taji.

Mechi itapigwa saa 4;45 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Wawili Mbaroni Kwa kupanga Shambulizi la Kigaidi Mkesha wa Mwaka Mpya
Pep Guardiola Amekuja Kupumzika Afrika