Mijadala ya nani ni msanii wa hip hop namba moja nchini iliyoibuka hivi karibuni, tangu MTV watoe orodha yao ambayo ilikumbana na maoni kinzani mitandaoni, imemfikia rapa Nikki wa Pili ambaye amefunguka maoni yake.

Rapa huyo ambaye ni mmoja kati ya wasanii wanaounda kundi la Weusi aliiambia Ladha 3600 ya E-FM wiki hii kuwa kumtaja msanii ambaye ni namba moja kunategemea na mtazamo binafsi na namna ulivyoviweka vigezo vyako.

Mbali na uwezo mkubwa wa kughani, Nikki wa Pili amesisitiza umuhimu wa kigezo cha nyimbo za msanii husika kuwafikia watu wengi zaidi katika kumvisha taji la kuwa namba moja.

Alisema hata MTV kwenye orodha yao ambayo hata yeye pia alitajwa, waliangalia vigezo vyao ambavyo vinaweza visiwe sahihi kwa mtazamo wa mtu mwingine.

“Na mimi nasema kwamba tunapopima ukali tusibague, tuweke vigezo vingi. Sawa unatakiwa uwe mkali lakini pia inatakiwa muziki wako uwe unafikia watu wengi kwa sababu hiyo ndio dhana,” Nikki alifunguka.

“Huwezi kusema kwamba ‘mimi ni MC mkali’ halafu watu hawaifahamu kazi yako. Kwa sababu wewe mwenyewe umejikosea, kwa sababu sanaa yako hujashare na watu wengi. Kama unaweza kujirahisisha kwa namna fulani… kama beat fulani na chorus fulani inaweza kusaidia ukawafikia watu wengi zaidi kwanini usifanye hivyo,” aliongeza.

Hivi karibuni kwenye mtandao wa Instagram ulizuka mjadala mzito baada ya mhariri mkuu wa mtandao wa Bongo5, Fredrick Bundala kueleza kuwa anavyoona kwa sasa Darassa ndiye msanii wa hip hop namba moja Tanzania kwani nyimbo zake tatu zote alizotoa zimekuwa hit kubwa.

Maoni hayo yalimkuna sikio Nash MC ambaye aliyapinga kwa nguvu huku akidai kuwa aliyetajwa hata kwenye orodha ya wana-hip hop hayumo.

Serikali kuwawashia moto wanaokwamisha uboreshaji wa sekta binafsi
Lema asusia maisha ya uraiani, mkewe alia na vikwazo