Mzunguuko wa tatu wa ligi kuu ya England utakamilishwa rasmi hii leo kwa mchezo mmoja kuchezwa mishale ya saa nne usiku kwa saa za Afrika mashariki, ambapo Manchester United watakua wenyeji wa Tottenham Hotspurs kwenye uwanja wa Old Trafford.

Wawili hao watakutana usiku wa leo, huku kila mmoja akiwa na hamu ya kuibuka na ushindi kufuatia matokeo ya michezo ya mzunguuko wa pili, ambapo kwa upande wa wenyeji Man Utd walikubali kupoteza dhidi ya Brighton and Holve Albion kwa kufungwa mabao matatu kwa mawili, huku Spurs wakihitaji kuendelea na ushindi baada ya kuwakandamiza Fulham maboa matatu kwa moja.

Kuelekea mchezo huo, mshambuliaji kutoka nchini Chile Alexis Sanchez anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Man Utd, baada ya kukosa mchezo uliopita dhidi ya Brighton kufuatia majeraha ya nyama za paja yaliyokua yakimsumbua.

Kiungo Nemanja Matic na Antonio Valencia pia wanapewa nafasi kubwa ya kurejea kikosini baada ya kupona majeraha.

Kwa upande wa Spurs, tayari meneja Mauricio Pochettino ameshathibitisha kuendelea kumkosa Son Heung-min ambaye bado ana majukumu ya kuitumikia timu yake ya taifa ya Korea Kusini katika michuano ya Asian Games.

Kiungo kutoka nchini Kenya Victor Wanyama mwishoni mwa juma lililopita alirejea mazoezini sambamba na wachezaji wenzake na huenda akawa sehemu ya kikosi kitakachoanza hii leo.

 

Kauli za Mameneja:

Meneja wa Man Utd Jose Mourinho: “Mchezo wetu dhidi ya Brighton, tunakubali tulifanya makosa na tukaadhibiwa, hatuna budi kujirekebisha katika mchezo unaofuata dhidi ya Spurs, ambao tutaucheza tukiwa katika himaya ya nyumbani.”

“Naamini mchezo wa soka una matokeo ya kushangaza, labda mambo huenda yakaendelea kuwa mabaya kwa mara nyingine tena mbele ya Spurs, lakini tutajitahidi kupambana hadi kuhakikisha kila mmoja anaondoka uwanjani akiwa na furaha.

“Msimu uliopita tulifanikiwa kufanya vizuri katika michezo mikubwa kama hii, ninaamini hata msimu huu hali itaendelea kuwa hivyo, kikubwa ni wachezaji kujituma na kutambua umuhimu wa mchezo husika.”

Meneja wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino: “Nasi ni sehemu ya klabu kubwa katika ligi ya England, tunapaswa kuheshimiwa na kuwaheshimu wengine. Tutakwenda uwanjani huku tukitambua tunacheza na timu ya aina gani, lakini lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunapata ushindi ambao utatuongezea pointi tatu.

“Katika soka historia ina nafasi yake, lakini kwa kipindi hiki siamini tena katika historia, kwa sababu kila timu imejiandaa vizuri na inahitaji matokeo, lakini kama tutaendeelea kuamini historia, hakutokua na haja ya kupambana na kuweka matumaini ya kupata ushindi.”

“Kwa miaka ya nyuma Spurs walipata tabu sana katika uwanja wa Old Trafford ndivyo historia inavyosema, lakini kwa sasa tunahitaji kuiendeleza historia kwa namna tofauti ya kupata ushindi.”

Katika msimamo wa ligi Man Utd wanashika nafasi ya 9 kwa kuwa na alama 3, na Spurs wanashika nafasi ya 6 kwa kuwa na alama 6, huku kila mmoja akiwa ameshashuka dimbani mara mbili.

Chadema waanza kulia rafu mapema Monduli, Lowassa asogea
Video: Goodluck Gosbert asimulia alivyopata mualiko Ikulu