Mshambuliaji kutoka nchini Ivory Coast Nicolas Pepe ameombwa kujifunza kukabiliana na changamoto za ligi kuu ya England, ambayo ameanza kuichezea msimu huu, baada ya kusajiliwa na washika bunduki wa kaskazini mwa jijini London.

Ushauri huo kwa Pepe, umetolewa na meneja wa Arsenal Unai Emery, kufuatia udhaifu waliouonyesha wakati wa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Manchester United uliomalizika kwa sare ya bao moja kwa moja, siku ya jumatatu.

Pepe, aliyesajiliwa kwa dau la Pauni milioni 72, amekiri kwamba amekuwa hajiamini kabisa kwa kipindi cha hivi karibuni na hivyo kumfanya acheze kwa kiwango duni hususan katika mchezo huo, ambapo alipoteza mipira mara 17.

Emery amesema mshambuliaji huyo hana budi ajifunze kukabiliana na presha ya ligi ya England, ili kufanikishja makali yake kama alivyokua Ufaransa na klabu ya Lille.

Huko Lille, Pepe alifunga mabao 23 msimu uliopita na hivyo kuwashawishi Arsenal kwenda kunasa huduma yake tena wakilipa mkwanja mrefu ulioweka rekodi huko Emirates.

“Wachezaji nao ni wanadamu, tunacheza michezo kila siku, kama meneja au mchezaji ni lazima kuwa kwenye presha. Lakini, unapaswa kuichukulia presha kwa mtazamo chanya. Kuwa kwenye presha ni kawaida kwa sasa, sisi ni klabu kubwa na tumekuwa na mahitaji makubwa. Hilo ndilo la msingi na si kuzungumzia pesa.” alisema Emery.

Pepe ameshafunga bao moja katika michezo saba aliyocheza, tangu kuanza kwa msimu huu.

Video: Utata RC kuwacharaza bakora wanafunzi 14, Giza ghafla lang'oa kigogo wa Tanesco
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 4, 2019