Kikosi cha timu ya taifa ya Nigeria kimekamilika kambini, tayari kwa mchezo wa kuwania nafasi ya kufuzu fainali za mataifa ya barani Afrika za mwaka 2017, dhidi ya Misri utakaochezwa mwishoni mwa juma hili.

Kikosi cha taifa hilo ambalo limewahi kutwaa ubingwa wa Afrika mara tatu (1980, 1994 na 2013) kimekamilika baada ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa huko barani Ulaya na Amerika kujumuika na wenzao, tayari kwa mchezo huo, utakaochezwa kwenye uwanja wa Ahmadu Bello, mjini Kaduna.

Jumla ya wachezaji tisa ambao wanacheza nje ya Nigeria waliwasili kambini usiku wa kuamkia hii leo huko mjini Abuja na tayari asubuhi hii wameanza mazoezi na wenzao, ambao walijikusanya baada ya michezo ya ligi ya mwishoni mwa juma lililopita.

Mshambuliaji wa klabu ya West Ham Utd ya nchini England, Victor Moses na chipukizi wa klabu ya Manchester City, Kelechi Iheanacho ni miongoni mwa wachezaji waliofika kambini huko mjini Abuja.

Wachezaji wengine waliopo ni mshambuliaji wa klabu ya Portland Timbers ya nchini Marekani, Fanendo Adi pamoja na mlinda mlango Carl Ikeme anayeitumikia klabu ya Doncaster Rovers akitokea Wolverhampton Wanderers, zote za England.

Wachezaji wengine wanaocheza nje ya Nigeria waliowasili kambini ni Alex Iwobi, Mikel Obi, Odion Ighalo, Aaron Samuel na Umar Aminu.

Wanaocheza ligi ya nchini Nigeria waliopo kambini ni Ifeanyi Matthew, Kalu Orji, Chibuzor Okonkwo, Ikechukwu Ezenwa, Oghenekaro Etebo pamoja na Etim Matthew.

Wachezaji Wa Azam FC Kupumzika Kwa Siku Kadhaa
Mmiliki Wa Newcastle Utd Atoboa Siri Ya Kumuajiri Benitez