Mweusi Nikki wa Pili ameliuza Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) maswali kuhusu utaratibu wa kufungia kazi za wasanii nchini akihoji kwanini hawakuwahi kuzifungia nyimbo za matusi wakati wa uchaguzi.

Rapa huyo msomi ambaye alikutana uso kwa macho na Katibu wa Basata, Godfrey Mngereza kwenye mjadala maalum kwenye kipindi cha The Playlist cha Times Fm ulioongozwa na Lil Ommy, alitaka kufahamu pia sababu za kuufungia wimbo wa Young Dee, ‘Bongo Bahati Mbaya’.

Akijibu maswali hayo, Mngereza alimtaka Nikki kutambua kuwa wakati wa uchaguzi kuna mamlaka zinazosimamia uchaguzi kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Kuna nyimbo wanasema iko katika package ya masuala ya uchaguzi. Na wanaotoa kibali cha kipi kifanyike na kipi kisifanyike sio Basata. Na wanazungumza kabisa, walitoa waraka kuwa wakati wa kampeni kusiwe na nyimbo za matusi,” Mngereza alimjibu Nikki.

Hata hivyo, Nikki alionesha kutoridhishwa na majibu hayo akihoji kuwa kama angetoa nyimbo inayohusu siasa wakati huo Basata wangekuwa likizo? Swali ambalo alijibiwa kuwa NEC ndio wangekuwa na mamlaka ya maudhui ya uchaguzi.

Kuhusu kufungiwa kwa ‘Bongo Bahati Mbaya’, ingawa Nikki alimtetea Young Dee kuwa alikuwa na ndoto yake inayowakilisha maono yake kuwa ‘Hollywood’ yake ni Masaki akimaanisha alitamani maisha ya watanzania wengi yangekuwa kama yalivyo ya Masaki, alijibiwa kuwa kuwaacha vijana wafikirie hivyo ni kama kuwaacha watu wasambaze ndoto zao kuwa ‘bora wangezaliwa mbwa Ulaya’.

Wafugaji waua wakulima watano kwa risasi
Video: Asasi ya Fedha kuwakomboa vijana katika matumizi ya fedha