Rapa mweusi, Nikki wa Pili sio mtu wa ‘mchezo-mchezo’ kwakuwa anamiliki kipaji cha aina yake kinachofanana na cha Jay Z kinachowaacha wengi midomo wazi akiwa studio.

Nikki amefunguka kupitia The Playlist ya 100.5 kuwa ingawa amekuwa akitengeneza ngoma kali na mitindo mikali isiyotabirika kama ‘Kiburi Flow’, kwa kiasi kikubwa amekuwa haandiki mashairi yake kokote, bali hutunga kichwani na kukariri kisha kurekodi kilichotunzwa kichwani kwake. Uwezo ambao amedai ulimchanganya mtayarishaji mkongwe wa muziki, P-Funk Majani.

Rapa huyo autaja wimbo wa ‘Kiujamaa’ uliotikisa akimshirikisha Pipi. Alisema utunzi wa wimbo huo ulianzia kwenye mitindo huru hadi kuikamilisha kwa kuiweka sawa kichwani kabla hajatema moto kwenye studio za mtayarishaji Mona Gangster.

Uwezo huo wa kutunga mashairi kwa kichwa, kuyakariri na kurekodi kisha kuwa wimbo mkubwa anao rapa Jay Z. Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika, Jay Z hajawahi kuandika mashairi ya wimbo wake kokote hususan tangu mwaka 1999. Jigga huandikia kichwani na kutengeneza hits kubwa unazozisikia kama ‘Empire States of Mind’.

“Mara nyingi mimi huwa naandika kichwani, naandika kichwani na-memorize. Nadhani kwa sababu ya shule. Nakumbuka kipindi fulani P-Funk aliniambia ‘mbona huna daftari wala nini’, nikamwambia mimi huwa naandika kichwani…Majani alikuwa anachanganyikiwa,” Nikki wa Pili aliiambia The Playlist ya 100.5 Times Fm.

Hivi karibuni, Nikki wa Pili ameachia wimbo mpya alioubatiza jina la ‘Quality Time’, aliomshirikisha G-Nako.

Mbali na marapa hao, Saida Kalori pia amekuwa akieleza kuwa hajawahi kuandika wimbo wake wowote kwenye karatasi, bali hutunga kichwani na kukamilisha masuala yote kichwani. Hata hivyo, uwezo wa aina hii ni mgumu zaidi kwa marapa ambao hutumia mistari mingi na mitindo mingi kwenye shairi moja.

Unaweza kuangalia interview nzima ya Nikki wa Pili hapa:

Video: LHRC walaani shambulio la walemavu, wataka Jeshi la Polisi DSM liombe radhi
Mtoto aliyekuwa anakunywa mafuta, sukari na maziwa aruhusiwa MNH