Kiungo wa Young Africans Haruna Niyonzima amesema wakati huu ligi ikiwa imesimama, anaendelea kujiweka sawa tayari kwa kuisaidia timu yake pale ligi itakaporejea.

Pamoja na kutekeleza program ya mazoezi ya timu, nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Rwanda amesema kila siku jioni hufanya mazoezi ufukweni akijumuika na wachezaji wa timu mbalimbali.

“Kwa kawaida asubuhi tunafanya mazoezi ya timu, jioni najumuika na wachezaji wa timu nyingine kufanya mazoezi hapa ufukweni.”

“Tunafanya mazoezi mchanganyiko ikiwa ni pamoja na kukimbia, kucheza mpira muhimu kujenga stamina na kuongeza pumzi ili wakati ligi itakaporejea tuwe sawasawa.” amesema Niyonzima

Niyonzima amekuwa na mwanzo mzuri katika awamu yake ya pili kunako klabu ya Young Africans aliyojiunga nayo mwezi Januari 2020.

Kwa mara ya kwanza Niyonzima alisajiliwa na Young Africans mwaka 2012, akacheza kwa misimu mitano kisha kujiunga na Simba mwaka 2017 ambako alicheza kwa misimu miwili.

Alirejea Young Africans akitokea klabu ya AS Kigali ya kwao Rwanda ambayo aliitumikia kwa miezi sita tu.

Yacouba Sogne awekwa njia panda
Makame: Kukaa benchi kunanipa chahu ya kupambana