Kiungo kutoka Rwanda na klabu ya Young Africans Haruna Niyonzima ameeleza kuvutiwa na uchezaji wa kiungo anayecheza nae kikosi cha mabingwa hao wa kihistoria, Mapinduzi Balama.

Niyonzima aliyerejea Young Africans mwezi Januari, amesema Balama ni mmoja wa wachezaji bora aliowahi kucheza nao “Navutiwa sana na uchezaji wa Mapinduzi Balama. Nafikiri akiendelea kujituma atapata mafanikio makubwa sana. Ni mchezeji mwenye kipaji na anapokuwa uwanjani anafahamu vyema majukumu yake,” amesema Niyonzima.

Niyonzima aliongeza kuwa bao alilofunga nyota huyo kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Simba Januari 04 mwaka huu, ni miongoni mwa mabao bora yaliyofungwa msimu huu.

Balama alisajiliwa Young Africans mwanzoni mwa msimu akitokea klabu ya Alliance Fc ya jijini Mwanza, alianza vyema maisha yake Jangwani akijihakikishia nafasi kwenye kikosi cha kwanza licha ya mabadiliko ya makocha watatu.

Kiwango chake kimempa nafasi ya kuitwa kikosi cha timu ya Taifa kilichopaswa kushiriki michuano ya CHAN nchini Cameroon, ambayo hata hivyo iliahirishwa kutokana na janga la Corona.

Hostel za wanafunzi UDSM kutumika kama karantini
Aliyemng’oa Gadaffi madarakani afariki kwa corona