Uwezekano wa kiungo Haruna Hakizimana Niyonzima kuichezea klabu yake, Yanga SC Jumamosi Dar es Salaam dhidi ya Azam FC ni mdogo.

Niyonzima ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ amefunga ndoa ya serikali mjini Kigali, Rwanda. Amefunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu ambaye pia ni mzazi mwenzake ambaye sasa wana watoto watatu.

Katibu wa Yanga SC, Dk. Jonas Tiboroha ameithibitishia kwamba, Niyonzima bado hajawasili.

“Niyonzima hajawasili, nadhani anaweza kuja kesho, kwa sababu walikuwa Morocco na timu yao ya taifa,”amesema Dk. Tiboroha.

Katibu huyo wa Yanga SC amesema mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe amewasili tangu juzi na leo amefanya mazoezi na wenzake Uwanja wa Boko Veterani, Dar es Salaam.

Yanga SC imeweka kambi hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani Pwani na inafanya mazoezi, uwanja wa Boko Veterani nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Azam FC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Aidha, kiungo Mnyarwanda wa Azam FC, Jean Baptiste Mugiraneza naye pia hajarejea Dar es Salaam, hivyo yuko hatarini kuikosa mechi hiyo ya kukata na shoka.

Lowassa Ashangaa Alichokisema Rais Kikwete
Nahodha Wa Yanga Arejesha Salamu Chamazi