Msongo wa mawazo kazini ni kitu kinachowasumbua wafanyakazi wengi zaidi na hata wengine hufikia hatua ya kuchukia kazi husika hata kama ina malipo mazuri kutokana na changamoto mbalimbali za kikazi.

Hata hivyo, njia sahihi ya kuishi na kuongeza kipato chako ukiwa na furaha ni kujitahidi kufanya kazi na kuepuka njia zinazoweza kukuletea msongo wa mawazo kwa sababu za kikazi, kuliko kutafuta namna ya kuondoa msongo huo. Kinga ni bora kuliko tiba.

Leo nitakueleza njia tano za kukwepa kupata msongo wa mawazo kazini.

  1. Yasome vizuri mazingira ya kazi yako na kufuata mdundo

Kila ofisi ina mazingira yake na namna inavyojiendesha. Ili usiingie katika msongo wa mawazo anza kuyasoma mazingira ya kazi yako kwa umakini mkubwa kwa kufuatilia mikataba yako, kuwafahamu vizuri maboss na walio chini yako kitabia na namna wanavyofanya kazi. Mfahamu kila mmoja unaefanya nae kazi ili umtengenezee picha ya namna ya kuishi naye vizuri. Hii itakusaidia kuepuka kushtukizwa kwa maamuzi usiyoyategemea au kauli usizotegemea kutoka kwa mtu husika. Unapoona mambo yanakuwa magumu, ishi kwa mujibu wa mazingira husika ya kazi. Yaani fuata mdundo wa muziki unaopigwa lakini kuwa muangalifu sana usiingie kwenye mtego.

  1. Timiza majukumu yako kwa ufanisi na kwa wakati, wasiliana kwa kujiamini

Jitahidi kutimiza majukumu yako kwa muda na kwa wakati ili kuepusha kutokubalika kazini kwa kuchelewesha mambo. Unaweza kuhisi unasumbuliwa na boss wako, kumbe wewe ni chanzo cha usumbufu huo.

Hakikisha unaweka mezani mambo aliyokuagiza kwa wakati na kwa ufanisi kadiri uwezavyo. Hii itakusaidia kutoingia kwenye maudhi ya lugha ambazo hazitakufurahisha na kukunyima amani mwisho kukupa msongo wa mawazo.

  1. Jiamini

Amini kuwa wewe ndiye unayefaa kufanya kazi husika, amini ofisi uliyopo hukuipata kwa kubahatisha hivyo ufanisi wa kazi zako na CV yako ndivyo vinavyokubeba. Hii itakufanya kufanya kazi yako kwa kujiamini (lakini usipitilize). Usiamini kuwa kazi hiyo ndiyo iliyobeba maisha yako yote, bali amini ndiyo iliyobeba stamina ya uchumi wako kwa wakati huo na unaihitaji sana. Hii itakufanya kufanya kazi kwa bidii kupata unachotaka ili upige hatua kimaisha kuliko kufikiria kuwa hakuna maisha nje ya hiyo kazi. Hivyo, hii itakufanya kuwajibika zaidi na kuitunza ‘mood’ yako pale unapovurugwa.

  1. Sikiliza, Tafakari, Uliza, Tekeleza

Ili ukwepe msongo wa mawazo na kupenda mazingira ya kazi yako, unapaswa kumsikiliza kwa makini mteja au mtu yoyote anayezungumza na wewe mambo ya kazi. Sikio lako lisibague usikivu kwa kuangalia anayeongea ni nani. Kila linalozungumzwa kuhusu kazi ni muhimu sana kwani ukiteleza kupitia hilo litakuletea matatizo ambayo yanaweza kuanza kidogo na kulipuka kuwa chanzo cha msongo wa mawazo kwa kuhisi unasakamwa ofisini.

Attentive Listening

Jifunze kusikiliza zaidi ya kuongea,tafakari ulichosikia na uliza swali kujiridhisha kile ulichoelekezwa ili mambo yako yaende sio tu kwa sababu umeambiwa ufanye bali ulichoambiwa na matokeo yanayotarajiwa.

Hii itakusaidia pia kujenga uhusiano mzuri kati yako na wafanyakazi wenzako na mwisho kuunda urafiki zaidi ya uadui.

  1. Kuwa na mtazamo chanya

Kuwa na mtazamo chanya juu ya mambo yanayoendelea ofisini. Usichukulie kila unachoambiwa na usichokipenda kuwa ni sehemu ya tatizo na manyanyaso kwako. Ichukulie kwa mtazamo chanya, unapovuka kikwazo ndio chanzo cha kuongeza uaminifu zaidi kwa wakuu wako wa kazi.

Kumbuka, huwezi kuitwa bora kwa njia ya mteremko tu, ubora wako hupimwa pia na namna unavyozikabili changamoto zako ofisini. Usizigeuze changamoto za ofisi kuwa matatizo. Hii itakupelekea kuwa na msongo wa mawazo unaotokana na changamoto za ofisi husika.

Watuhumiwa Upotevu wa Makontena 349 Wapandishwa Kizimbani
Kilichoipeleka Azam FC Tanga Chafahamika