Klabu ya Sevilla imemrejesha nchini Hispania mshambuliaji Manuel Agudo Durán (Nolito), akitokea Manchester City ya England kwa ada ya Pauni milioni 7.9.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30, amerejea nyumbani kwao Hispania na kusaini mkataba wa miaka mitatu.

Nolito alisajiliwa na Man City mwishoni mwa msimu wa 2015/16 akitokea Celta Vigo ya Hispania, na aliaminiwa na Pep Guardiola huenda angefanya vyema katika kikosi chake, lakini ilikua tofauti licha ya kumaliza msimu uliopita kwa kufunga mabao matatu.

“Ninafuraha isiyo kifani, hadi najihisi kuchizika kwa kufanikisha mpango wa kurejea tena katika ligi ya Hispania, nilitamani kuendelea kubaki Man City lakini imeonekana inafaa mimi kurejea hapa nyumbani,” Amesema Nolito.

“Ninafurahishwa na soka linalochezwa hapa Hispania, nilipokua England nilijifunza utamaduni mwingine wa soka na nilijaribu kufanya kila lililowezekana, lakini imenibidi kurudi hapa na ninaahidi nitacheza kwa uwezo wangu wote.

“Naamini furaha nilionayo hata kwa mashabiki wa Sevilla nao wapo hivyo, ninatarajia ushirikiano mkubwa tutakaouonyesha dhidi ya wachezaji wenzangu, tufafanikisha jambo kubwa mwishoni mwa msimu wa 2017/18.”

Klabu ya Sevilla ambayo ilimaliza msimu uliopita ikiwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ya Hispania, ilikua ikitafuta mshambuliaji wa kati ambaye angeziba nafasi iliyoachwa wazi na Víctor Machín Pérez (Vitolo) aliyesajiliwa na Atletico Madrid kwa Euro milioni 36 ambazo ni sawa na Pauni milioni 31.5, juma lililopita.

Vitollo atacheza kwa mkopo kwenye klabu ya Las Palmas hadi mwezi Januari mwaka 2018, ambapo adhabu ya kufungiwa kusajili ya Atletico Madrid iliyotolewa na FIFA itakua inamalizika.

Associazione Calcio Milan Yakamilisha Kwa Lucas Biglia
Joe Hart Kufanyiwa Vipimo Vya Afya