Mashabiki na Wanachama wa Young Africans wameombwa kufika mapema Uwanja wa Benjamin Mkapa, ili kuwa sehemu za sherehe maalumu ya klabu hiyo kutimiza miaka 86.

Wito kwa Mashabiki na Wanachama wa Young Africans umetolewa na Afisa Mhamasishaji Antonio Nugaz, ambapo amehimiza wahusika kufika uwanjani hapo kuanza majira ya saa 11:00 jioni kabla kikosi chao kumenyana na Kagera Sugar, majina ya saa moja usiku.

Nugaz amesema Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo ni sehemu ya mafanikio ya Young Africans, hivyo kufika kwao kutaendelea kudhihirisha umoja na mshikamano uliodumu miongoni mwao kwa miaka mingi.

“Mashabiki na Wanachama ndio wenye klabu yao, hawana budi kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa ili kusheherekea uzao wa Young Africans ambayo imefikisha umri wa miaka 86.”

“Tukifika kwa wingi na kushiriki katika tukio la sherehe yetu, tutadhihirisha umoja na mshikamano wetu uliodumu kwa miaka mingi, hivyo kila mmoja ninamsisitiza afike bila kukosa.” Amesema Nugaz

Baada ya sherehe hizo wachezaji wa Young Africans watakuwa na kazi ya kusaka alama tatu muhimu mbele ya Kagera Sugar inayonolewa na Kocha Mkuu, Mecky Maxime.

Kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Kaitaba, Young Africans ilishinda bao 1-0, hivyo leo kazi itakuwa kubwa kwa timu zote mbili kusaka ushindi.

Mchezo wao wa ligi uliopita Young Africans ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Mbeya City huku Kagera Sugar ikiwa imetoka kupata sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Gwambina FC.

Makala: Yafahamu Maisha ya Maalim Seif, milima na mabonde
Simba SC yatinga Musoma, Mara