Mwimbaji Nuru The Light ameyakumbuka maisha matamu ya penzi la miaka mitano yaliyogeuka shubiri ghafla na jinsi alivyoyaweka kwenye wimbo wake mpya ‘Umeniacha’. Mpenzi wake huyo hakuwa mtu maarufu.

Akifunguka hivi karibuni kwenye The Playlist ya 100.5 Times FM, mwimbaji huyo ambaye alifanya vizuri na ‘Muhogo Andazi’ akiwa na Bob Junior, ‘Nisubiri Usilale’, ‘Chapa Lapa’,’ #L’ na nyingine nyingi amesema kuwa wimbo wake huo aliouandika kwa kuzingatia simulizi la kweli la uhusiano wake wa mapenzi unaweza kuwa tiba mojawapo kwa watu wengine wanaoachwa na wapenzi wao bila kutarajia, kuona kuwa maisha mazuri zaidi yanaweza kuwa mbele yao.

Ameeleza kuwa baada ya kuachwa aligundua aliyekuwa naye hakuwa baraka yake kwani milango ilifunguka na akaanza kuona fursa zaidi mithili ya madini ya almasi.

“Unajua kuna mwingine labda kaachwa anaona kama ‘Mungu wangu maisha ndiyo yameisha’…. lakini kuna watu nuksi, nilikuwa na mmoja huyo (anacheka)…! Kwa sababu tulipoachana milango ikafunguka na ghafla nikaanza kuona roses (maua waridi), nikaona Diamonds (almasi), yaani kila kitu kikawa ‘on fire’,” alifunguka.

Aliongeza kuwa kwenye uhusiano wa mapenzi ni vyema watu wakafahamu kuwa hata kuachwa pia huwa kunakuja na baraka nyingine.

Nuru The Light ni moja kati ya waimbaji wa Bongo Fleva wa muda mrefu. Takriban miaka kumi iliyopita tayari alikuwa na nyimbo zilizofanya vizuri.

‘Walimwengu’, ‘Msela’, ‘Chapa Lapa feat. Vedasto’, na nyingine zilimpa nafasi kwenye anga ya Bongo Fleva. Wimbo wake ‘Muhogo Andazi’ ni moja kati ya nyimbo zilizofanya vizuri kabla ya kuhamishia makazi yake ya kwa muda nchini Sweden akifanya kazi kama mtaalam wa ushauri wa masuala ya kisaikolojia.

Serikali yaitahadharisha Simba
Dkt. Mwakyembe awasihi Watanzania kumsaidia Wastara