Aliyewahi kuwa Mbunge wa Singida Kaskazini kupitia Chama cha Mapinduzi CCM na baadaye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu amefafanua tuhuma kutoka katika miandao ya kijamii kuwa alidanganya idadi ya kura alizopata kutoka kwa Kamati Kuu ya CHADEMA wakati wa mchakato wa kutafuta Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

Akizungumza katika kipindi cha Mahojiano alichofanya na Kituo cha Utangazaji cha Star TV, Nyalandu amefafanua kuwa alikuwa sahihi katika maelezo yake aliyoatoa katika kipindi cha mahojiano alichofanya hivi karibuni akieleza kuwa alipata kura 30 za Kamati Kuu dhidi ya Tundu Lissu aliyepata Kura 24.

Nyalandu ameeleza kuwa wakati wa mchakato walikuwa wagombea Saba na walipigiwa kura na wajumbe 30 wa Kamati Kuu ambapo kila Mjumbe aliruhusiwa kuwapigia kura wagombea watatu.

“Tulikuwa wagombea kadhaa, nadhani Saba, so kura ya kwanza ilipigwa Kamati kuu ya CHADEMA, kamati kuu ya CHADEMA ina watu 30, kwa hiyo kuna kura 30, wagombea walikuwa 7 kwa hiyo utaratibu wa Chama ilikuwa ni lazima kila mjumbe apigie (kura) watu watatu, kwa sababu wanaopelekwa walikuwa lazima wawe watatu kati ya saba,” amesema Nyalandu.

“Katika zile kura tatu ambazo kila mtu alikuwa anatakiwa kupigia watu watatu tofauti ilikuwa lazima mtofautiane tu hizo kura, na ndio nikasikia ubishi kwa watu ambao walikuwa wanajua hizo ni propaganda tu, hivyo baada ya matokeo mimi nikapata asilimia 100, nakumbuka nilipata kura 30, Bwana Lissu kura 24, kulikuwa na dada mwingine alikuwa na kura sikumbuki idadi yake lakini mimi niliwaongoza kwa mbali wote,” ameeleza Nyalandu.

“Shida iliyokuwepo ni kwamba ndo haya mambo ya huyu CCM isije ikawa hivi, wakaamua matokeo yawe siri lakini tupeleke majina matatu, yakapigiwe kura, nadhani hiyo ilikuwa ni… wazungu wanaita ‘ommision’, ilikuwa ni kushindwa kwa chama kuonyesha umahiri wake wa kutetea demokrasia ya wazi ndani ya chama kwa sababu kura zikipigwa huwa sharti zitangazwe,” amefafanua Nyalandu.

Nyalandu ameeleza kuwa baada ya Baraza Kuu kukaa liliamu jina la Lissu lipitishwe kuwa Mgombea Urais uamuzi ambao yeye kama Mwanachama kwa wakati huo alikubaliana nao.

Hivi karibuni Nyalandu kupitia kipindi cha Mahojiano alichokifanya na kituo kimoja cha habari alinukuliwa akisema, “Wakati nakwenda kwenye kamati kuu ya CHADEMA wajumbe walikuwa 30 nilipata kura zote Tundu Lissu alipata Kura 24, nilimgalagaza kwelikweli. Watu wakasema Nyalandu asije akawa kama Lowassa, watu waliotoka CCM hatuwezi tukawaamini,” kauli ambayo ilizua mijadala iliyolenga kuonyesha kuwa Nyalandu alidanganya kutokana na mkanganyiko wa takwimu za uwepo wa wajumbe 30 na kura 54.

Nyalandu ameeleza kuwa safari yake ya CHADEMA ilikuwa na mitihani mingi huku akikishauri Chama hicho kujifunza kutokubezana wenyewe kwa wenyewe au wageni wanaowapata.

TRA yafungulia akaunti zote za wafanyabiashara ilizozifungia
Rais Samia apokea ujumbe maalum wa Rais wa Burundi